Na Baraka Mbolembole
MABINGWA mara moja wa zamani, Azam FC inapaswa kupandisha kiwango chao kiufungaji msimu huu na mchezo wa raundi ya saba ugenini vs Mbao FC unapaswa kuambatana na tumakini mkubwa katika kujilinda kwani timu hiyo ya Mwanza inapenda kushambulia sana ikicheza katika uwanja wa Kirumba.
Mbao FC japokuwa haijapata ushindi wowote katika uwanja wao wa nyumbani lakini kiufungaji kikosi hicho cha kocha Mrundi, Etienne kimefanikiwa kufunga magoli manne katika uwanja wa Kirumba dhidi ya Simba SC na Mbeya City FC huku mshambulizi wake Habib Hajji akiwa tayari ameshafunga magoli matatu kati ya nane ya timu yake.
Beki ‘yanya’ ya Mbao, wafungaji butu Azam FC
Mlinzi wa kulia, Boniphace Maganga amefunga magoli mawili hadi sasa. Stahili yake ya kupanda kuongeza nguvu katika mashambulizi na umakini wake katika kupiga mashuti ya mbali yenye mwelekeo sahihi ulimfanya mlinzi huyo chipukizi wa Taifa Stars kufunga goli la ushindi wakati Mbao FC ilipopata ushindi pekee msimu huu vs Kagera Sugar FC (ugenini).
Mlinzi wa kati na nahodha wa kikosi hicho Mrundi, Yusuph Ndikuma amefunga goli moja na kufanya safu hiyo ya ulinzi kuwa na idadi kubwa zaidi ya magoli ya kufunga hadi sasa wakati ligi ikiwa imeshachezwa michezo sita kwa kila timu.
Kiuzuiaji, Mbao FC ni timu ya tatu iliyoruhusu magoli mengi katika ligi msimu huu (imefungwa magoli tisa.) Wakati safu hiyo ya ulinzi ya kikosi cha Etienne ikiruhusu magoli tisa, safu ya mashambulizi ya kikosi cha Mromania, Aristica imefunga magoli matano tu.
Mbaraka Yusuph ndiye kinara wa ufungaji wa Azam FC hadi sasa akiwa amefunga magoli mawili. Mghana, Yahaya Mohamed amefunga goli moja sawa na kijana Peter Paul ambaye alifunga goli la kusawazisha wakati Azam FC ilipolazimisha sare ya 1-1 dhidi ya Singida United. Huku nahodha wa kikosi, Himid Mao akifunga katika sare iliyopita Mwadui FC 1-1 Azam FC.
Kitendo cha washambuliaji hao kufunga magoli manne katika michezo sita kwa timu inayojengwa bado nasisitiza wako katika mwendo mzuri na kwa kutumia udhaifu wa Mbao FC katika kujilinda kikosi hicho kilichotwaa ubingwa msimu wa 2013/14 kinaweza ‘kunoa’ makali zaidi kwa kufunga walau magioli mawili katika mchezo mmoja kwa mara ya kwanza msimu huu.
Mbio za ubingwa ni sasa
Kuwa na pointi 12 sawa na viongozi wa ligi Simba SC, MtIbwa Sugar na mabingwa watetezi kunaonyesha kuwa ligi bado ‘mbichi’ nab ado hakuna tofauti kubwa kati ya timu na timu.
Kwa Azam FC ambao walianza maandalizi yao Juni na kuwa timu ya kwanza kufanya hivyo sasa wanapaswa kuanza kufunga kweli ili kuthibisha kuwa wako tayari kwa mbio za ubingwa na pengine kushinda taji hilo kwa mara ya pili mwishoni mwa msimu.
Kushindwa kupata matokeo ya ushindi katika michezo vs Singida United ( Jamhuri Stadium, Dodoma) na Mwadui FC (Mwadui Complex) bado hakupaswi kuwakatisha tama kwani wamekutana na timu ambazo pengine zingiweza kuwafunga bila Azam FC kukomboa goli katika kila mchezo.
Ila timu yenye dhamira ya ubingwa inapaswa kushinda walau mchezo mmoja na kutoa sare mbili katika viwanja vya ugenini. Lakini bahati mbaya kwa Azam FC wanaweza kushindwa kupata ushindi katika mchezo wa tatu mfululizo wakicheza ugenini kwa sababu wanakutana na Mbao ambao pia wanasaka ushindi wa kwanza nyumbani msimu huu.
Kumbuka Mbao FC nao wanaingia katika mchezo huu vs Azam FC Jumamosi hii wakipambana kuepeka sare ya tatu mfululizo katika uwanja wa nyumbani. Nani mshindi?