Young Dee
BIFU baina ya wasanii si jambo geni kwenye tasnia ya muziki duniani. Asilimia kubwa ya wanamuziki waliowahi kuwa, au waliopo kwenye ushindani mkali mara kwa mara wamejikuta ndani ya bifu linalotokana na ushindani wao au kutengenezwa na wapenzi wa kazi zao! Jambo linalosisimua zaidi unaweza kukuta wanamuziki hao wanaokuwa kwenye bifu kali walikuwa ni marafiki wakubwa, waliokula, kunywa na kulala pamoja.

Lakini kutokana na maslahi umaarufu pamoja na kutunza heshima kwa kila mmoja wao wanajikuta katika bifu kali. Miongoni mwa bifu zilizowahi kutikisa ni baina ya wakali wawili wa Muziki wa Hip Hop, Tupac Shakur na Biggie Small ‘B.I.G’ ambao wote kwa sasa ni marehemu.

Washikaji hawa kabla ya kuingia kwenye uhasimu mkubwa unaosemwa na wachambuzi mbalimbali wa masuala ya burudani Marekani kwamba ndiyo ulisababisha vifo vyao, walikuwa marafiki wakubwa baada ya kukutana kwa mara ya kwanza huko Los Angeles, mwaka 1993! Kilichofuata baada ya kukutana kwao ni ushikaji wa damu kiasi kwamba kila Biggie alipokuwa akienda California alilala nyumbani kwa Tupac na kila Tupac alipokwenda New York alilala kwa B.I.G huko Brooklyn.

Wakaimba pia pamoja kwenye matamasha mengi likiwemo lile la Budweiser Superfest lililofanyika kwenye Ukumbi wa Madison Square Garden, mwaka 1993. Hata hivyo urafiki wao uliingia dosari baadaye baada ya B.I.G kukua kimuziki zaidi na kuwa mshindani wa rafiki yake Tupac ambaye alikuwa anafanya vizuri kwenye muziki na muvi kabla hata ya kukutana kwao. Bifu hilo baadaye lilihusishwa kwenye vifo vyao, wote walikufa kwa kupigwa risasi, Tupac ndiye alianza mwaka 1996, akafuata B.I.G mwaka 1997.

Si hao tu, kwenye historia ya muziki kumeshuhudiwa bifu za wasanii zilizotikisa kwelikweli kama Nas na Jay Z, Jay Z na marehemu Prodigy, Nicki Minaj na Miley Cyrus, Meek Mill na Drake, Kanye West na Jay Z, Casper Nyovest na A.K.A (kutoka Afrika Kusini).

Mbali na Marekani na Afrika Kusini ambako nimegusia kidogo, hapa nyumbani wasanii mbalimbali wamekuwa wakiumana vikali kuanzia kwenye makundi ya muziki mpaka mwanamuziki mmoja mmoja.

Ukiachana na hilo, bifu nyingine ambazo zimewahi kuteka hisia za mashabiki wa muziki Bongo kutokana na sababu mbalimbali ni Dudu Baya na Mr Nice, Q Chief na T.I.D, Langa na Jay Moe, Godzillah na Wakazi, Nay wa Mitego na Nick Mbishi, Muumin Mwinjuma na Ally Choki, kwa sasa Nandy na Ray C hapatoshi huku Young Killer na Young Dee nao wakivimbiana! Kuhusu Ray C na Nandy bifu lao limeanza hivi karibuni baada ya Nandy kutumbuiza nyimbo za Ray C kwenye Matamasha ya Tigo Fiesta yanayoendelea.