KILIO CHETU KWA WAAMUZI BADO KINAENDELEA
KUNA wakati tunasema kuna aibu za kujitakia tu hilo linatokana na kama unafanya jambo la hovyo wakati ulikuwa na uwezo wa kuliepuka. Ni watu wengi tu au taasisi nyingi hapa nchini zinafanya makosa ya kujitakia na kupata aibu ambazo wangeweza kuiepuka.
Jumamosi iliyopita nilikuwa mmoja ya watazamaji, nilienda kuangalia mechi ya kirafiki baina ya Taifa Stars dhidi ya timu ya taifa ya Malawi na nilichokiona huko kutoka kwa muamuzi, ninamuachia mwenyezi Mungu.
Sijui waamuzi wetu wanakumbwa na pepo gani? Mara nyingi najiuliza hili swali lakini ninakosa jibu kabisa. Hawa ndugu zetu bado wanatupa shida sijui wataendelea hivi hadi lini? Maana tumeshawachoka na kuharibu kwao lakini hawabadiliki miaka nenda miaka rudi.
Kwenye michezo ya ligi zetu hapa nyumbani kama Ligi Daraja la Kwanza au Ligi Kuu Tanzania Bara tumeshazoea huko kuharibu kwao lakini inapofika hadi kwenye michezo ya kimataifa hapo inatupa shaka zaidi.
Ninasema hivyo kwa kuwa inatupa shaka sababu watu wamekuwa wakisema eti waamuzi wetu wanafanya vizuri mno wakichezesha mechi za kimataifa na sasa Mungu alituonyesha uongo wao mbele yetu.
Tulipata aibu mbele ya Wamalawi wale wachache waliokuwepo uwanjani kisa mtu mmoja tu aliyesimama katikati kuhukumu mchezo ule na akashindwa kuifanya ile kazi ipasavyo na hilo ndiyo tatizo.
Sijui tufanye nini ili waamuzi wetu waweze kutuelewa sijui hawajui kama wanatukera kwelikweli na tumechoshwa na huko kuvurunda kwao kila siku.
Hapo juu nilianza kwa kusema kuwa ni aibu ya kujitakia, ni kweli nilichokiona ni aibu ya kujitakia kwa wakuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa sababu walikuwa na uwezo mkubwa wa kuleta mwamuzi kutoka nje ya nchi kuchezesha mchezo huo, hata kama inegkuwa kutoka nchi jirani tunazopakana nazo.
Basi kama ingeshindikana kabisa wangechukua waamuzi kutoka Zanzibar na siyo waamuzi hawa wa huku Bara ambao wengi wao tunawajua maana kuvurunda kwao imekuwa ni sehemu ya maisha yao yaani hakuna jipya.
Kwa mfano kocha wa Malawi siku ile alitolewa kwenye benchi kwa kuililia haki yake na wote tuliona lazima tuseme kweli na tumuogope mwenyezi Mungu.
Mpira ulitolewa na mmoja ya wachezaji wa Taifa Stars, ilibidi iwe kona lakini muamuzi yule akawanyima kona Malawi ndipo kocha wao alipoanza kulalama kuililia haki yake na kwa kujisafisha ndugu yangu muamuzi akaamua kumtoa kwenye benchi na kumpeleka jukwaani kwa mashabiki.
Kwa ufupi mimi nimeshawachoka hawa waamuzi wetu basi tu sina la kufanya lakini wanayoyafanya kwenye soka letu ni madudu matupu ambayo hayawawezi kuvumilika hata kidogo.
Mwisho kabisa naomba msalimieni Salum Mayanga na mwambie kazi njema ya kuendelea kujenga timu na sijui tutakuwa tunajenga timu hadi lini? Lakini ndiyo hivyo tuendelee kupambana na hali zetu.
Nadhani Mayanga atakuwa amejifunza kitu kwenye mchezo ule dhidi ya Malawi kama wanavyosema Waswahili kuwa ‘Wali wa kushiba unaonekana kwenye sahani’.
Post a Comment