KESI YA LULU KUHUSISHWA NA KIFO CHA KANUMBA KUANZA KUUNGURUMA
MSANII maarufu wa kike wa fani ya uigizaji wa filamu nchini, Elizabeth Michael Kimemeta, ‘Lulu’, anayekabiliwa na kesi ya mauaji ya aliyekuwa msanii maarufu wa kiume wa fani hiyo, Steven Kanumba, keshokutwa atapanda kizimbani tena wakati kesi hiyo itakapoanza kuunguruma.
Lulu ambaye yuko nje kwa dhamana anakabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, akidaiwa kumuua Kanumba bila kukusudia, kinyume cha Kifungu cha 195 cha Kanuni za Adhabu (PC), April 7, 2012, nyumbani kwa marehemu Kanumba, Sinza Vatican.
Kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam vya mashauri ya jinai, kesi hiyo itasikilizwa keshokutwa na Jaji Sam Rumanyika kuanzia keshokutwa, Alhamis Oktoba 19 hadi Jumatatu Oktoba 23, mwaka huu.
Wakati upande wa mashtaka (Jamhuri) ukidai kuwa Lulu alimuua Kanumba bila kukusudia, hata hivyo Lulu mwenyewe wakati wa usikilizwaji wa awali mahakamani ambapo alisomewa maelezo ya kesi hiyo alikana mashtaka hayo ya kuua bila kukusudia.
Hivyo kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa kuanzia keshokutwa, upande wa mashtaka utakuwa na wajibu wa kuwaita mashahidi mahakamani kutoa ushahidi na hata vielelezo kuthibitisha kuwa msanii huyo alitenda kosa hilo.
Hata hivyo ikiwa mara hii atakiri kosa hilo, basi Jamhuri haitalazimika kuita mashahidi wake kuthibitisha kosa hilo bali mahakama itamtia hatiani tu kwa kukiri kwake na kisha kumhukumu adhabu ambayo itaona kuwa inafaa.
Mshtakiwa anayepatikana na hatia ya kosa la kuua bila kukusudia, adhabu ya juu huwa ni kifungo cha Maisha adhabu ya chini huwa ni kuachiwa huru kabisa, kutegemea na mazingira ya kesi husika.
Kwa hiyo mahakama inaweza kumhukumu mshtakiwa kifungo cha maisha, miaka 20, mitano, mwezi, siku, saa ama kumwachia huru kabisa.
Lulu alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza April 10, 2012, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa shtaka la kumuua Kanumba, lakini hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria kusikiliza kesi za namna hiyo, isipokuwa Mahakama Kuu.
Februari 17 msanii huyo alipandishwa kizimbani Mahakama Kuu na kujibu mashtaka hayo kwa mara ya kwanza, wakati wa usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo (PH), ambapo alisomewa maelezo yote ya kesi inayomkabli.
Siku hiyo Lulu alikubali kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Kanumba, jambo ambalo ni miongoni mwa mambo manane ambayo aliyakiri mahakamani hapo, kama mambo yasiyobishaniwa katika kesi hiyo, lakini akakana kumuua Kanumba bila kukusudia.
Mambo mengine ambayo Lulu aliyakiri mahakamani hapo yaliyoko katika maelezo ya kesi hiyo ni pamoja na jina na anuani yake, kwenda nyumbani kwa Kanumba usiku wa tukio hilo, kuwa na ugomvi na Kanumba pia Kanumba kumzuia kutoka nje ya chumba alipojaribu kutoka ili akimbie.
Mengine ni kufanikiwa kutoka nje ya chumba cha marehemu Kanumba, kumweleza mdogo wa Kanumba (Seth Bosco) kuwa Kanumba ameanguka, kukamatwa kwake na polisi eneo la Bamaga, saa 11 Alfajiri ya usiku wa tukio hilo na kushtakiwa kwa kosa la kumuua Kanumba bila kukusudia.
Baada ya Lulu kukana mashtaka, Wakili wa Serikali, Monica Mbogo aliiarifu mahakama kuwa wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, upande wa mashtaka utakuwa na mashahidi wanne.
Aliwataja mashahidi hao kuwa ni pamoja na Seth Bosco, Daktari binafsi aliyekuwa akimhudumia Kanumba, Dk Paplas Kageiya, Ester Zephania na Askari D/Sgt Ernatus wa Kituo cha Polisi Oysterbay.
Pia Wakili Mbogo aliwasilisha mahakamani vielelezo viwili vitakayotumika kama sehemu ya ushahidi katika kesi hiyo ambayo ni taarifa ya kitabibu ya uchunguzi wa chanzo cha kifo cha Kanumba na ramani ya eneo la tukio.
Lulu kwa upande wake, mawakili wake Peter Kibatala na Fulgence Massawe waliiarifu Mahakama kuwa wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo kwenye utetezi watakuwa na mashahidi watano na vielelezo viwili. Hata hivyo hawakutaja majina ya mashahidi hao.
Post a Comment