Header Ads

MSIMCHUKULIE POA ARSENE WENGER


Jose Mourinho.
LIGI Kuu England ipo raundi ya tatu tangu ianze msimu huu huku Manchester United, iliyo chini ya Jose Mourinho, ikiwa kileleni kwa pointi zake tisa. Mashabiki kote duniani wanaofuatilia michuano hiyo, wameshaanza ubashiri na tayari wameshamuondoa Arsene Wenger katika orodha ya makocha watakaomaliza ligi hiyo kwa kicheko.
Hiyo inafuatia matokeo ya mechi zake tatu za awali, kwani imeambulia ushindi mara moja tu, dhidi ya Leicester City huku ikikubali vipigo viwili mfululizo, vyote ugenini dhidi ya Stoke City na baadaye nyumbani kwa Liverpool, ambayo ilimpa pigo kubwa, baada ya kumpeleka kambani mara nne bila majibu.
Mashabiki wengi wa Arsenal na hata timu pinzani, zimekuwa zikimuona Wengerkama ndiye tatizo namba moja kwa klabu hiyo kushindwa kutwaa mataji ya Ligi Kuu, tangu ilipofanya hivyo msimu wa 2003/04 ambao pia aliweka rekodi ya kumaliza michuano hiyo bila kupoteza hata mechi moja.
Anasemwa kwa ubahiri wa kununua wachezaji, kwamba ndicho kikwazo kikubwa cha yeye kushindwa kutengeneza kikosi imara cha kuwania mataji, karibu wote wakikubaliana kuwa huu ni wakati muafaka wa kumtaka kuondoka katika klabu hiyo aliyojiunga nayo mwaka 1996.
Kwa mashabiki, wanaweza kuwa wako sawa kwa sababu lengo lao siku zote ni timu yao kutwaa taji, lakini hali haiko hivyo ndani ya bodi ya klabu, kwa sababu wao lengo lao ni kuona thamani ya klabu yao ikiongezeka, hivyo hisa zao kuzidi kutuna.
Ubahiri wa Wenger unainufaisha timu hiyo, ndiyo maana siku zote wakurugenzi na wamiliki wamekuwa nyuma yake kila anapokutana na wakati mgumu kama huu. Hata hivyo, Wenger siyo kocha mbaya kiasi hicho, kwani ndiye ambaye ameifanya Arsenal kuwa klabu kubwa duniani na kutengeneza mashabiki wengi.
Mashabiki wanamkataa tu kwa sababu wanadhani amehudumu kwa muda mrefu, lakini wanasahau kuwa aina ya soka linalochezwa na timu hiyo, halipatikani miongoni mwa klabu nyingi England.
Akiwa na kikosi cha bei rahisi, kwa zaidi ya miaka 20 mfululizo, kocha huyu ameiwezesha timu hiyo kuwemo ndani ya Nne Bora kila msimu unapomalizika na hivyo kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya, kitu ambacho timu nyingi zimeshindwa. Kwa kushiriki michuano hiyo mikubwa kabisa ngazi ya klabu, kunamaanisha kuipa fedha nyingi zaidi timu hiyo.
Kuna klabu zinazotumia mamilioni ya pauni kununua wachezaji wa bei mbaya duniani kote, lakini zimeshindwa kuifikia rekodi hii ya kucheza Ligi ya Mabingwa kwa muda wote huo mfululizo. Na historia ya timu hiyo katika England, inaonyesha wazi kuwa huwa inaanza kwa kusuasua, lakini kadiri muda unavyosonga mbele, ndivyo inavyozidi kuwa imara zaidi.
NA: OJUKU ABRAHAM| IJUMAA

No comments