THE PLAYLIST YA TIMES FM: MSIMU MPYA WAZINDULIWA KWA KISHINDO!
NI Shiida! Unaweza sema hivyo kwa maana nyingine baada ya kuzinduliwa kwa kishindo msimu mpya wa shoo bab’kubwa ya burudani kwa vijana Bongo, THE PLAYLIST inayoruka kupitia kituo cha Redio cha Times FM (100.5) chini ya mtangazaji mwenye mbwembwe nyingi, Omary Tambwe ‘Lil Ommy’.
Katika shoo hiyo ya kibabe mjini, msimu mpya wa mageuzi ulizinduliwa rasmi Agosti 7, mwaka huu katika Lounge na Garden ya Times FM, Kawe jijini Dar huku mastaa kibao wakihudhuria wakiwemo watangazaji, washereheshaji, wasanii na wauza nyago kwenye video mbalimbali za Kibongo ‘video queens’.
Miongoni mwa wakali waliohudhuria uzinduzi huo uliokuwa na bata za kutosha kama vile kukata keki, kuchoma nyama na kunywa vinywaji ni Amber Lulu, MC Pilipili, Jigga Low, DJ Choka, Magie Vampire, Angel Merikato, Taiya, Foby pamoja na Prodyuza Duppy.
Msimu waja na mapinduzi
Akizungumza na global publishers, Lil Ommy alisema tangu kuanza kwa kipindi hicho mwaka 2013, kilikuwa kikiruka kila siku ya Jumamosi na Jumapili lakini msimu kimekuja tofauti ambapo kitakuwa kikiruka kuanzia siku ya Jumatatu hadi Ijumaa.
“The Playlist ni moja kati ya vipindi pekee vinavyotikisa Bongo. Baada ya maombi mengi ya wasikilizaji wetu kuomba muda zaidi suala hilo tumelifanyia kazi na sasa kwa mara ya kwanza katika historia ya kipindi hiki kitakuwa kikiruka rasmi kuanzia siku ya Jumatatu hadi Ijumaa saa 8 mchana hadi saa 12 jioni tofauti na zamani kilianza kuruka Jumapili tukabadilisha ikawa Jumamosi na sasa ni siku za kazi (weekdays),” alisema Ommy.
Vipengele vyaongezwa
Ommy aliongeza kuwa safari hii The Playlist imeboresha zaidi kuanzia siku hadi vipengele.
“Kuna vipengele tumeongeza kwenye shoo ambavyo ni INBOX ambapo utakuwa kama uwanja wa vijana kutuma maoni yao, pia kipengele kingine ni INDUSTRY BUZZ ambayo ni sehemu ya kupata habari za burudani huku kipengele kingine cha JIONGEZE kikiwa maalumu kwa kupata maujanja ya mjini na kuwa macho usiingie chaka.”
Ngoma 5 kama kawa!
Ommy aliongezea kuwa, kipengele pendwa cha misimu yote cha mastaa kuja kuchangua ngoma 5 kali wanazozikubali kitaendelea kuwepo palepale.
“Kipengele cha ngoma 5 kali anazokubali staa hakijabadilika ila kimeboreshwa ambapo kwa sasa watakuwa wanakuja mastaa wengi zaidi kwenye shoo kuliko zamani.”
Watangazaji waongezeka
Ommy alimalizia kuwa katika kuboresha kipindi hicho kinachotoka Jumatatu hadi Ijumaa, kipindi kimeongezwa mtangazaji pamoja na DJ.
“Tutakuwa na Dj J One na mtangazaji mwingine wa Kike, Kattie ambao wataipamba shoo vilivyo,” alimaliza Ommy na kusisitiza kuwa shoo hiyo ni kila Jumatatu hadi Ijumaa kuanzia saa 8 mchana hadi Saa 12 jioni kupitia 100.5 Times FM.
Post a Comment