‘Kiroho safi, Mzee Kilomoni kaondoe kesi mahakamani, iache Simba iende inapotakiwa…
Na Baraka Mbolembole
ILI kufikiriwa kusamehewa na wanachama wengi wa klabu, kwanza Mzee Hamis Kilomoni anapaswa ‘kutokwa’ na mawazo yake kuwa ‘hawezi kuondolewa’ katika nafasi ya mwenyekiti wa Baraza la wadhamini klabuni Simba, nafasi ambayo alivuliwa jana Jumapili katika mkutano mkuu wa mwaka wa klabu.
Akubali mabadiliko
Wakati fulani nilikuwa ‘mpinga’ mabadiliko ya klabu ya Simba. Nilipinga kwa sababu sikupendezwa na baadhi ya ‘nyendo’ za baadhi ya waliokuwa viongozi wa juu wa klabu hiyo wakati suala la mabadiliko ya mfumo wa kiuendeshaji klabu kutoka katika utegemezi wa wanachama na kujiendesha katika mfumo wa soko la hisa.
Nilisema, upande wangu pia nilikuwa nahitaji kuona ‘Simba ya ndoto zangu,’ lakini nilikuwa na mitazamo miwili chanya na nimewahi kuielezea katika makala zangu zilizopita.
Naamini katika mabadiliko ya klabu kuingia katika soko la hisa lakini si kwa haraka ambayo waliitaka wanachama Agosti mwaka uliopita. Naamini suala la kubadilisha mfumo uliodumu kwa miongo zaidi ya nane (zaidi ya miaka 80) si jambo la mara moja.
Wakati huohuo niliona Simba inaweza kujiendesha kibiashara hata ikibaki katika mfumo wa kutegemea wanachama, ila ni hadi pale wanapoweza kupatikana watu ambao wanataka maendeleo ya kweli katika klabu na timu ndani ya uwanja.
Mabadiliko ya mfumo wa kiuendeshaji yanaweza kuwa hatua maalumu ya mafanikio kuelekea ukombozi wa kweli wa mpira wa miguu Tanzania ambayo wengi tunayahitaji.
Niliandika sana kuhusu udhaifu wa wanachama wakati wa chaguzi za klabu ya Simba na nilipowauliza maswali kadhaa muhimu kuhusu machaguo yao, waliniita ‘kibaraka wa Yanga.’ Sikutumia njia mbaya lakini kwa kile kinachoendelea kuhusu baadhi ya viongozi wa juu wa klabu hiyo, naamini nitaeleweka siku moja, hata kama sitaitwa ‘mwenzao.’
Mwaka mmoja sasa tangu suala la mabadiliko klabuni Simba, naamini mambo mengi yamerekebishwa huku serikali ikiwa kando ya mchakato huo hivyo naamini umefika wakati wa Mzee Kilomoni na wale ambao tuliamini mwanzo mchakato huo kutokwenda inavyotakiwa, sasa tuamini mabadiliko yajayo yanakidhi wakati tuliopo, wataalamu na Serikali wamehusika.
Kiroho safi Kilomoni kaondoe kesi mahakamani
Simba itabaki ya wanachama daima, lakini si kwa kutegemea mchango wa Mzee Kilomoni tena bali mawazo yake. Naamini mamlaka zinampatia mtu mamlaka ndizo zinazoweza kumuondolea mamlaka husika.
Kilomoni ameondolewa katika nafasi yake ya mwenyekiti wa baraza la wadhamini na kusimamishwa uanachama kwa sababu amefungua kesi mahakamani kupinga mkutano ujao wa mabadiliko ya katiba ni kosa si kwa katiba ya Simba tu bali hata FIFA haipendezwi na masuala ya soka kupelekwa mahakamani.
Sifa kubwa ya mwanadamu ni ‘kufanya makosa’, kukosea ndiyo ubinadamu kwa maana hakuna mkamilifu. Bado haujachelewa, Mzee Kilomoni ‘kiungwana’ tu, kaondoeni kesi mahakamani. Iacheni Simba sasa ikatengeneze maisha na ajira nyingi kwa vijana wa kitanzania.
Post a Comment