FAHAMU UMUHIMU WA KULA MBOGA MBICHI (SALADI)
KUNA watu wanapokwenda hotelini huagiza saladi tu. Salad ni mkusanyiko wa mboga za majani mabichi. Kinachotakiwa kujulikana ni kuwa ulaji wa mbogamboga zikiwa katika hali ya ubichi au zikiwa hazijapikwa una faida kubwa kiafya.
Hata hivyo, ulaji huo bila ya kuchukua tahadhari unaweza kusababisha magonjwa yanayoenea kutokana na kula vyakula vichafu visivyosafishwa vema. Katika maisha ya binadamu karibu kila jambo zuri linatakiwa kufanywa kwa tahadhari au kuchunga miiko yake, bila ya kufanya hivyo, faida ya jambo hilo haitapatikana na badala yake mtu anaweza kukumbwa na maradhi.
Ulaji wa mbogamboga zikiwa katika hali ya ubichi au zikiwa hazijapikwa una faida kubwa kiafya. Hata hivyo, ulaji huo bila ya kuchukua tahadhari utasababisha magonjwa yanayoenea kutokana na kula vyakula vichafu. Ni ukweli wa miaka mingi kuwa kupika au kutumia moto katika kuandaa vyakula kunaharibu virutubisho vya asili vinavyopatikana katika mbogamboga.
Mboga za majani kama mchicha, matembele, kisamvu, spinachi na kadhalika ambazo hazijakomaa na mbichi ni chanzo kikubwa cha vitamini na madini ya aina mbalimbali. Mboga hizo endapo zitakamuliwa na kutumiwa kama juisi, faida yake kiafya itakuwa kubwa hasa kwa wagonjwa.
Mbogamboga zinaondoa tindikali inayozalishwa wakati vyakula vingine vikisagwa tumboni kama vile nyama na jibini. Mboga za majani za kijani ni chanzo kikubwa cha carotene ambayo inabadilishwa mwilini na kuwa vitamini A. pia, ni chanzo kizuri cha vitamini C.
Vitamini A ina kazi kubwa ya kuimarisha macho ili yaone vizuri hasa wakati wa giza na ndiyo maana wapo wanaoshauri kula mchicha kwa wingi kama hawaoni vizuri hasa kama giza limeingia. Vitamini A. Mbogamboga pia, inasaidia pia ukuaji na ufanyaji kazi wa chembehai na kuimarisha kinga ya mwili.
Vitamini C ina kazi nyingi ikiwemo kuimarisha ufanyaji kazi wa chembehai, inaimarisha kinga, kuponya mafua na vidonda. Baadhi ya mbogamboga zina protini na wanga. Kwa mfano, maharage na kunde ni chanzo kikubwa cha madini ya chuma na protini.
Viazi mviringo na viazi vitamu ni chanzo kikubwa cha wanga mwilini. Siku hizi kuna kuongezeka kwa tabia ya watu kutumia mboga zikiwa mbichi kutokana na wengi kutambua umuhimu wake. Tunawahimiza watu watumie mboga mbichi kama vile saladi na kachumbari wakati wanapopata milo yao.
Wanaweza kuzitumia zikiwa zimekatwakatwa au kusagwa ili kupata juisi, lakini ni lazima kuzingatia usafi wakati wa kuandaa mboga hizo.
USHAURI
Kwa ushahidi wa kutosha wa kisayansi, ulaji wa vyakula vibichi ambavyo havikuoshwa vizuri ni chanzo kikubwa cha magonjwa ya kuambukiza kama vile homa ya matumbo, kipindupindu, tumbo la kuhara, kuhara damu, kupata minyoo na amiba.
Kwa sababu hiyo, watu wanashauriwa kuosha vizuri mbogamboga kwa kutumia maji safi na salama. Pia, watu wale saladi na wanywe juisi ya mboga mbichi ili kupata virutubisho vingi zaidi. Mbogamboga kama matango, nyanya na karoti, zitumike kutengeneza juisi bila ya kuondoa maganda yake. Kwa sababu maganda yana madini na protini kwa wingi
UMAKINI
Watu wawe makini kujua mahali zilipozalishwa mbogamboga wanazizonunua. Miaka michache iliyopita, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kiliwahi kufanya tafiti mbalimbali kuhusu ubora wa mbogamboga zinazozalishwa kandokando ya barabara zinazopita magari au katika bonde la Mto Msimbazi au mito mingine jijini Dar es Salaam. Tafiti hizo zilibaini kuwa baadhi ya mboga zilikuwa hazifai kuliwa na binadamu wala wanyama kutokana na kuwa na kemikali zinazodhuru afya hivyo ni muhimu kuwa makini.
NA: MWANDISHI WETU| UWAZI JUMANNE
Post a Comment