Kurasa nne za Stereo hadi tunapomsoma WCB
Stereo ni rapper ambaye kwa sasa mkononi anashikilia albamu moja inayokwenda kwa jina la Africa Son aliyoitoa mwaka 2012 akiwa chini ya usimamizi wa M Lab.
M Lab walikuwa na kundi lilojulikana kama Lundono ambapo alikuwepo Stereo, One the Incredible na Nikki Mbishi lakini hapa baadae umoja huo ulivunjika baada ya Stereo kujitoa kwa sababu zake binafsi. M Lab kwenye mikono ya Duke Tachez ndio mwanzao wa Tamaduni Muziki na kilinge, hivyo Stereo nae alikuwa wa pande zote mbili.
Crew ya Tamaduni Muziki ambayo ina msimamo wake, uandishi na vionjo vyake katika muziki, na pia walikuwa wakosoaji wakubwa kwa aina fulani ya muziki Hip Hop ambao ulikuwa mainstream, tuachane na hilo. Stereo na wenzake, yaani Nikki Mbishi, One the Incredible, Nash MC, P the MC, Zaiidi, Mansu-li, Ghetto Ambassador, Songa, Dizasta, Malle na wengineo walikuwa waumini wakubwa wa beat za bum kubum na uandishi uliodeep sana.
Ukisikiliza nyimbo za Stereo za awali kama Nitabaki Juu, Rafiki, Chundabadi, Confidence, Swahili, Miss Chinese, Haina Ngwasu, Classic Material na nyinginezo utaelewa alikuwa wa namna gani. Lakini baadae alikuja kujitoa huko na kwenda sehemu nyingine ambapo alienda kuanzisha aina nyingine ya muziki ambayo naweza kusema ilikosolewa na wale waliokuwa wanaamini katika muziki wake wa awali.
Unity Entertainment
Mwaka 2012 alipata shavu la usimamizi wa kazi zake kwa miaka miwili chini ya management ya Unity Entertainment iliyokuwa chini ya AY, uwepo wake hapa ulimleta Stereo mpya katika kuandishi na namna ya kurap.
Ngoma ‘Usione Hatari’ aliyomshirikisha Ben Paul ilikuwa tofauti sana kwanzia beat, mashairi, video, flow ukilinganisha na nyimbo zake za awali. Haikuishia hapo pia ngoma yake Never Let You Down aliyompa shavu Victora Kimani kutoka nchini Kenya, ilitoa picha Stereo anataka kitu gani katika muziki wake.
Bila shaka alitaka muziki wake umnufaishe zaidi ya hapo awali, hivyo kubadilika huku ni kutafuta mashabiki wapya ili aweze kufanya biashara, ingawa kuna ambao wanapinga dhana hii. Mwisho wa siku muda wa kuwa chini ya Unity Entertainment ukamalizika na maisha mengine yakaendelea.
Kupeleka muziki wake Arusha
Kuna sababu iliyonifanya kuzungumzia part hii ila hapo mbele nitakueleza ni kwanini. Stereo anaingia katika vitabu vya kumbukumbu kwa kufanya kazi na baadhii wasanii wenye nguvu ya ushawishi katika muziki wa Hip Hop kwa pale Arusha.
Hapa nawazungumzia Mo Plus na Chindo Man kutoka Watengwa moja ya makundi ya Hip Hop yenye heshima yake pale Arusha. kazi waliyotoa watatu hawa ilikwenda kwa jina la Tindikali ambayo ilipikwa na prodyuza DX.
Sababu ya kuweka part hii kwamba katika crew ya Lundono kama sio Tamaduni Muziki kulikuwa na aina yao muziki waliokuwa wanauamini. Member wawili wa crew hizi, hapa nawazungumzia Nikki Mbishi na One the Incredible walikuwa wakosoaji wa muziki wa kundi la Weusi kutoka Arusha.
Katika hili ilifika wakati kukaripotiwa kuwepo beef kati ya Nikki Mbishi na Nikki wa Pili, One the Increble na Bonta, kitu kilichoanzisha mijadala katika mitandao ya kijamii na mtaani, eti katika muziki wa Tamaduni Muziki na ule wa Arusha upi ni mkali?. Katika mtandao wa facebook ilikuwa si ajabu kuona magroup yenye title Tamaduni Muziki Vs Arusha Hip Hop, tuachane na hilo.
Stereo na Nikki Mbishi ni marafiki wakubwa kwani licha ya kuwa chini ya label na kundi moja, wote wanatoka mtaa mmoja ‘Ukonga’, kwa mantiki hiyo kama ilivyo huluka ya binadamu ni lazima Stereo alikuwepo upande wa rafiki yake ingawa hakuonyesha hilo.
Sasa unaposikia Stereo ameenda kufanya kolabo na watu kutoka upande wa pili na unapata picha gani, lakini ni kwamba kuna sehemu alitaka muziki wake ufike na ndio maana sikushangaa niliposikia kolabo yake na G Nako ‘Sana’ iliyotoka mwaka jana.
WCB ukurasa mpya
Wiki hii tumesikia wimbo mpya wa Stereo ‘Mpe Habari’ ambao amemshirikisha Rich Mavoko, na wimbo huu umetengeneza na prodyuza Laizier kutoka Wasafi Records.
Stereo ameeleza kuwa siku ambayo Diamond na AY wanatambulisha Zigo Remix ndipo Diamond alisema Stereo ni miongoni ya msanii anaotamani kufanya nao kazi na habari zilipomfikia ndipo akamtafuta na walipokutana na kuzungumza akapata fursa ya kufanya kazi na msanii aliyechini ya label yake ‘Rich Mavoko’.
Sasa ngoma ya Stereo na Rich Mavoko inabamba mtaani ila haijajulikana kama Stereo amejiunga moja kwa moja na label ya WCB au yupo katika uangalizi, mwenyewe alipoulizwa kuhusu hilo alisema Babu Tale au Sallam ndio wanaweza kuliongelea zaidi na kuongeza, “Kimsingi WCB ni familia, hata sifikirii (kujiunga), yaani naona nimo tu, naona kama na mimi ni sehemu ya WCB”.
Twende mbele twende nyuma, vyovyote itakavyokuwa. Huu ni ukurasa mpya katika maisha ya kimuziki ya Stereo, wasanii wengine wanaweza kuusoma na kujifunza kitu. Sina maana wafanye kama yeye ila mtiririko wa kazi zake na hatua anazopiga zinaacha ujumbe mzuri.
Post a Comment