Header Ads

Roma: BASATA Nipunguzieni Adhabu Mtaniua Njaa







Siku chache baada ya Naibu Waziri wa Habari Sanaa, Michezo na Utamaduni, Juliana Shonza kusema wasanii waliofungiwa nyimbo zao wanatakiwa kufuata taratibu kama wana malalamiko, msanii wa Bongo Fleva, Ibrahim Musa maarufu  Roma Mkatoliki amesema alifuata taratibu hizo lakini amegonga mwamba.

Roma ameyasema hayo jana Jumatano Machi 21, 2018  katika mahojiano na kipindi cha XXL kinachorushwa na kituo cha Radio Clouds, akidai kuwa  adhabu ya kufungiwa miezi sita inamuumiza na kuomba apunguziwe au kutozwa faini ili yaishe.

Machi 1, 2018  Shonza alimfungia Roma Mkatoliki kutojihusisha na tasnia ya muziki kwa kipindi cha miezi sita na kwamba msanii huyo alipopewa muda wa kurekebisha wimbo wake wa Kibamia, ameshindwa kutekeleza agizo hilo.

Katika kipindi hicho, Roma amesema tangu siku alipofungiwa alijitahidi kufanya taratibu za kumuona naibu waziri huyo kama ambavyo alitaka, ikiwemo kufunga safari hadi ofisini kwake lakini  hakufanikiwa.

Amebainisha kuwa amefungiwa wakati tayari ana shoo za kufanya na alishachukua fedha, ikiwemo  shoo ya Kili Marathon ambayo baadaye alitakiwa kurejesha fedha hizo.

 “Shoo ya Kili Marathon mimi na Stamina kupitia kundi letu la Rostam tulikuwa tumelipwa vizuri, lakini juhudi za kufanikisha ziligonga mwamba hata kwa kuomba barua kidogo ya utambulisho. Mambo kama haya yanatuharibia kuaminika tena kwa kampuni ambazo zinatupa kazi,” amesema.

Kuhusu kumuona naibu waziri  amesema, “Siku moja nilitoka hospitali nikampitia rafiki yangu Madee na Askofu nikawaambia twendeni tukamuone mheshimiwa lakini mimi sikupewa ruhusa ya kumuona. Wengine wote walipewa ruhusa, basi nikawatuma wao wafikishe ujumbe kwa sababu niliogopa kulazimisha kwa kuwa ningeonekana nafanya fujo.”

Amesema alitakiwa kupewa muda kabla ya hatua iliyochukuliwa kuliko kudhaniwa kuwa anakaidi agizo la kutakiwa kuripoti ofisi za Baraza la Sanaa la Taifa (Basata).

“Walitakiwa kujua kuwa nilikuwa na udhuru na pia hiyo ilikuwa ni mara yangu ya kwanza,” amesema na kubainisha kuwa hata kama alipigiwa simu, aliogopa kupokea kwa sababu ya uoga alionao tangu alipotekwa na watu wasiojulikana mwaka jana.

“Inaonekana Roma hajafanya kitu chochote tangu litokee jambo hilo lakini ambacho mimi sijafanya ni kuja kwenye media kusema leo nimeandika barua au vipi? Sikupewa barua kwa wakati ule nilipewa ujumbe tena kwa namba ngeni.”

No comments