Header Ads

Mwananchi aliyejitolea kujenga zahanati kwa fedha zake, Amaliza na kuikabidhi Serikali



Emmanuel Mallya (katikati) akisaini hati na mkataba wa zahanati kwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Michael Kilawila kwenye hafla hiyo ya makabidhiano

Mfanyabiashara Emmanuel Mallya mkazi wa Moshi ambaye ametumia fedha zake kujenga zahanati ya kisasa na kuiwekea vifaa amemaliza zoezi hilo na rasmi ameikabidhi kwa serikali ili ianze kufanya kazi.

Ndg Mallya amesema aliamua kujenga zahanati hiyo baada ya kuona wakazi wa eneo la kijiji cha Uchau Kaskazini mwa wilaya ya Moshi Vijijini hususani akina mama wajawazito wakitembea umbali mrefu kutafuta huduma za afya kitu ambacho kimesababisha vifo vingi vya akina akina mama.
Hata hivyo, Ndg Mallya ametoa wito kwa watu wengine wenye uwezo kujitolea katika kuwahudumia wananchi kwa namna ama nyingine huku akidai kuwa kutoa sio lazima uwe na kitu kingi bali ni moyo.
Utajiri unatokana na moyo wa mtu alionao, unaweza ukawa na utajiri na usiwe na moyo wa kuwasaidia wengine, kila mtu amepewa karama na mwenyezi Mungu, muhimu hapa ni namna ya kuzitambua hizo karama.” amesema Mallya huku akiishukuru familia iliyokuwa ikiishi katika eneo ilipojengwa zahanati hiyo kwa kukubali kutoa ardhi hiyo na kupewa eneo jingine kubwa zaidi.
Kwa upande mwingine Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Mhe Anthony Komu, alihimiza usimamizi wa karibu wa zahanati hiyo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kippi Warioba .
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, uzoefu unaonyesha kuwa, miradi mingi inayojengwa na wafadhili imekuwa ikiharibika kutokana na kutokuwepo na usimamizi wa karibu, ni rai yangu kuwa tuitunze zahanati hii isijekuwa mazalia ya popo kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia kwa baadhi ya zahanati na vituo vya afya,” amesema Mhe Komu.
Kwa upande wa Serikali kupitia kwa Mkuu wa wilaya ya Moshi, Kippi Warioba umempongeza mfanyabiashara huyo kwa kusaidia watu wenye mahitaji na kutoa wito kwa wananchi kuachia baadhi ya maeneo ili zahanati hiyo ipanuliwe na kufika hadhi ya kituo cha Afya.
Chanzo:Mwananchi

No comments