Miaka 17 baada ya Kipanya Malapa, nani kuipa Yanga goli la kwanza Namfua ndani ya karne mpya?
Na Baraka Mbolembole
MIAKA 17 iliyopita, mshambulizi Kipanya Malapa ‘alizima’ isivyotarajiwa ndoto za Yanga kuizuia Mtibwa Sugar FC kuwa timu ya kwanza kutoka nje ya vilabu vikubwa Yanga na Simba kushinda ubingwa wa ligi kuu Tanzania Bara.
Mtibwa ilikuwa inatetea taji lake ililoshinda kwa mara ya kwanza mwaka 1999, na huku Yanga ikionekana kuwa timu pekee ya kuizuia kushinda ubingwa huo kwa mara ya pili mfululizo mwaka 2000, Kipanya akatokea kusikojulikana na kufunga goli pekee la ushindi kwa timu yake ya Singida United katika mchezo walioshinda 1-0 dhid ya Yanga katika uwanja wa Namfua, Singida.
Edibily Lunyamila, Akida Makunda, Sekilojo Chambua, Idd Moshi, Mohamed Hussein walikuwa wakiunda safu ya mashambulizi katika kikosi cha kocha Shungu lakini walishindwa kabisa kusawazisha goli la dakika ya 15 lililofungwa na Kipanya na Yanga wakachapwa na timu iliyoshuka daraja huku Mtibwa ikishinda taji lake la pili mfululizo na la mwisho katika historia yao.
Kutoka Novemba, 2000 sasa Novemba, 2017 Yanga watakwepa?
Mchezo wa kwanza wa ligi kuu baada ya kusubiri kwa miaka 17 katika uwanja wa Namfua utachezwa Jumamosi hii November 4, 2017 ambapo mabingwa mara 27 wa kihistoria-Yanga wanaenda kumkabili kwa mara ya kwanza kocha aliyewapa mataji mawili kati ya matatu mfululizo waliyoshinda ndani ya misimu mitatu iliyopita.
Raia wa Holland, Hans van der Pluijm aliweza kuipa Yanga mataji mawili ya VPL misimu ya 2014/15 na 2015/16 aliondolewa katika nafasi yake wakati ambao alikuwa mbioni kuipa timu hiyo ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo sifa ambayo baadae ilikwenda kwa Mzambia, George Lwandamina ambaye alichukua nafasi ya Hans mwezi Disemba, 2016.
Singida United imetumis pesa
Mlinzi wa kati, Salum Kipaga ni pekee ambaye anaweza kuanza katika kikosi cha Hans kati ya wachezaji ambao waliipandisha ligi kuu kwa mara nyingine Singida United mwezi April mwaka huu.
Hans ambaye amechukua nafasi ya Fred Felix Minziro ni kocha aliyefanya usajili mkubwa nyuma ya Simba. Magolikipa Ally Mustapha, Peter Manyika, wamesajiliwa na Hans msimu huu ili kusaidiana na Said Lubawa ambaye alikuwa chaguo la kwanza wakati timu hiyo ilipokuwa ikipambana kupanda VPL.
Uzoefu wa kucheza Simba na Yanga kwa zaidi ya miaka 13 mfululizo huku akishinda mataji lukuki alinao Mustapha na uzoefu alioupata Simba kwa misimu mitatu iliyopita unaweza kumsaidia Manyika na makipa hao wawili wakatengeneza ngome ngumu sambamba na walinzi, Salum Chuku, Mnyarwanda, Mishele Rusheshangoga, Shafiq Batambuze, Kenedy Juma na Kipaga.
Safu hii ya ulinzi imeruhusu magoli manne katika michezo nane iliyopita na wanakwenda kuwakabili washambuliaji wa Yanga huku wakijiamini baada ya kutoruhusu goli katika michezo mitatu mfululizo waliyocheza ugenini dhidi ya Ruvu Shooting (Mabatini, Mlandizi,) Ndanda FC (Nangwanda, Mtwara,) na Mtibwa (Manungu Complex, Turiani) ili kuvunja mwiko si tu wa kutoshinda Namfua Stadium katika karne mpya bali wa kufunga walau goli moja safu ya washambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa na Ibrahim Ajib inapaswa kuwa makini hata katika nafasi moja ambayo itapatikana kwani vijana wa Hans ni wagumu kufungika na wanacheza kwa kujiamini, kujituma na kutokubali kupoteza mechi kirahisi.
Timu hiyo imeshinda michezo miwili kati ya mitatu ambayo walikuwa wenyeji lakini yote walichezea Jamhuri Stadium, Dodoma kwa sababu uwanja wao wa nyumbani kiasili (Namfua) ulikuwa katika matengezo makubwa hasa eneo la kuchezea ambalo sasa kumepandwa nyasi za kisasa.
Kenny Ally, Deus Kaseke, Mzimbabwe. Tafadzwa Kutinyu na Kiggy Makasy wanaweza kuanza katika idara ya kiungo. Hans amekuwa akiwatumia wachezaji hao wanne katika mfumo wa 4-4-2 na licha ya kikosi chake kufunga magoli sita tu hadi sasa lakini bado viungo hao wamekuwa wakitoa msaada mkubwa kwa washambuliaji, Msauz, Katsavairo ambaye ameshafunga magoli mawili na aliyekuwa mfungaji bora mara mbili mfululizo wa ligi kuu ya Rwanda, Danny Usendimana ambaye ameshaifungia Singida United goli moja.
Yanga ni hatari ugenini
Tayari wameshachukua pointi kumi kati ya 12 katika michezo yao minne ya ugenini. Hans anafahamu vyema kuhusu uwezo wa Yanga katika kulazimisha matokeo wanapocheza ugenini na sitashangaa mabingwa hao watetezi wakienda Mbeya wiki ijayo wakiwa na alama 13 katika michezo mitano ya ugenini. Mcongoman, Papy Tshishimbi, Pius Buswita, Rafael Daud na Geofrey Mwashuiya wote walianza na kucheza vizuri katika mchezo uliopita vs Simba na kutokana na maendeleo ya majeraha ya Mzimbabwe, Thaban Kamusoko bila shaka kocha Lwandamina atamvaa ‘mtu aliyechukua’ nafasi yake klabuni Yanga miezi 10 iliyopita akiwa na viungo hao wanne.
Hassan Kessy anataraji kucheza mchezo wake wa pili msimu huu kutokana na Juma Abdul kusimamishwa kutokana na kupata kadi tatu za njano. Gadiel Michael katika beki ya kushoto, Vicent Andrew na Kelvin Yondan katika beki ya kati.
Post a Comment