MATONYA… DUDU BAYA, CHID BENZ, JIFUNZENI KITU
MATONYA ni jina la mwanamuziki mwenye heshima kubwa Bongo, amewahi kutamba na nyimbo nyingi zikiwemo Uaminifu, Siamini, Vaileti, Anita, Zilipendwa na ameshirikiana na wasanii wengi na wakali nchini.
Kwa muda aliokaa kwenye gemu la muziki wa Bongo Fleva, hutakosea ukimuita mkongwe au gwiji, si chini ya miaka kumi anapambana lakini mpaka leo jamaa bado anazidi kukomaa ili afike mbali na hapo alipo.
Hivi karibuni Matonya amechonga na Uwazi Showbiz dairekti kutokea nchini Kenya anakopalilia shamba lake.
Anapalilia shamba kwa maana yupo kwa ajili ya shughuli za kimuziki, akifanya kazi na baadhi ya wanamuziki wa nchini humo akiwemo Kaligraph Jones, lakini pia anafanya ziara kwenye media mbalimbali.
Ni jambo la kuvutia kuona mwanamuziki mkongwe kama Matonya akihangaika huku na huko ili kuzidi kujiimarisha na kuendelea kuwafikia mashabiki wake ambao wamekuwa wakimsapoti miaka nenda rudi.
Mbali na suala hili kuvutia ni somo pia kwa wakongwe wenzake wanaojaribu kufuta vumbi kwenye viti vyao na kurudi kwenye ‘trend’ ya muziki kama ilivyokuwa zamani.
Na hapa nawazungumzia kina Dudu Baya, Chid Benzi, Q Chillah, Jay Mo, Tid na wengine wengi.
Wanaweza kujifunza kitu kutoka kwa Matonya. Njia anazopita lakini hata kwa namna anavyojichanganya na wanamuziki wengine wenye ‘airtime’ zaidi kwa sasa kwenye media ndani na nje ya Bongo.
Matonya anaonesha malengo mazuri kimuziki kufanya kazi na Kaligraph Jones.
Unajua wakongwe wengi mara kadhaa wamekuwa wakifeli kuendelea kusimama au kurudi kwenye muziki kutokana na namna wanavyokuwa wanajirudisha au kuufanya muziki wao.
Kwa mfano hivi Dudu Baya ambaye alikuwa kimya muda mrefu kwenye gemu ameibuka kwa kufanya kolabo na Tid ya wimbo uitwao Inuka.
Si kazi mbaya, ni wimbo mzuri kabisa ambao wakongwe hao wote kwa namna zao wamejaribu kuonesha uwezo wao. Lakini kwa ushauri wangu, Dudu Baya kwa ujio huo na malengo yake ya kimuziki kurudi alipokuwa siku za awali hakuwa na haja ya kumshirikisha Tid ambaye na yeye kwa sasa hafanyi vizuri kihivyo.
Angetafuta wasanii wengine ambao ndiyo vinara wa hili gemu kwa sasa ili wakamsapoti kurudi juu, hata hivyo nampongeza Dudu kwa kuliona hili maana hivi karibuni nikipiga naye stori amesema yupo mbioni kuachia ngoma na Ben Pol pamoja na Bill Nas, tusubiri tuone!
Vivyo hivyo kwa Chid Benz kufanya kolabo na Q Chillah. Bado wanasomo la kujifunza kutoka kwa Matonya kwa kazi zao zinazokuja huko mbele, hawana haja ya kufanya kazi ilimradi kazi, au kazi na wanamuziki wanaowaamini wao kuwa ni bora wakati wapo pembeni na ‘trend’ ya muziki, kikubwa waangalie ubora wa mwanamuziki na nafasi yake kwenye muziki kwa sasa!
Post a Comment