Manchester United wanakwenda Anfield kuikabili Liverpool Jumamosi hii, mchezo ni mgumu na unataraji kuvuta hisia za watazamaji wengi ulimwenguni kutokana na upinzani na historia baina ya timu hizi mbili.
Wakati wachezaji na mashabiki wakijiandaa na mchezo huu kwa wiki hii, hali ni tofauti kwa kiungo mnyumbulifu wa Manchester United Juan Mata ambaye wiki hii alikuwa na ugeni mkubwa uwanjani Old Traford.
Juan Mata alisafirisha kundi la watoto maskini ambao wanacheza soka kutoka India akawaleta Uingereza ili kuja kuona Old Traford na kupiga picha katika maeneo mbali mbali ya uwanja huo na kujifunza kuhusu soka.
Ziara ya watoto hawa inakuja baada ya miezi michache iliyopita kiungo huyu alipotembelea mji wa Mumbai na kuona mazingira magumu wanayoishi watoto hawa na ndipo aliamua kuwaleta OT kama njia ya kuwahamasisha kufikia malengo yao.
Juan Mata ameamua kuwasaidia watoto hawa kwa kuwahamasisha kuhusu kucheza soka lakini pia kuwapa elimu ya maisha na darasani mpango ambao tayari baadhi ya nyota wakubwa duniani wameanza kumuunga mkono.
Juan Mata aliwaalika Ander Herrera na nyota wa zamani wa United anayekipiga Everton Morgan Schnerdelin kujumuika pamoja na watoto hao pamoja na kupiga nao picha kabla ya kuwapeleka katikati ya uwanja wa Old Traford.
Katika kuendeleza suala hilo Juan Mata amewaomba wacheza soka wenzake kuchangia hata 1% ya kipato chao ili kuwasaidia watoto wasio na uwezo huku akisema anaaamini wachezaji wenzake wa Manchester United watamuunga mkono.
Mlinzi wa Juventus Giorgio Chiellini amemtumia Juan Mata salamu za kumunga mkono kwa kile anachokifanya huku pia Matt Hummels wa Bayern Munich, Serge Gnabry wa Hoffnheim  nao wakiunga mkono kampeni hii ya Juan Matta.