Mshambuliaji wa Simba, John Bocco.
KOCHA Mkuu wa Simba, Joseph Omog, hana hofu ya kumkosa mshambuliaji wake John Bocco kwani tayari ameshampata mbadala wake atakayeanza katika mechi ya leo dhidi ya Njombe Mji.

Kauli hiyo, aliitoa jana kwenye mazoezi ya mwisho yaliyofanyika kwenye Viwanja wa Gymkhana jijini Dar es Salaam wakijiandaa na mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar.
Mshambuliaji wa kimataifa wa Simba raia wa Burundi, Laudit Mavugo.
Bocco ataukosa mchezo huo baada ya kupata majeraha ya kifundo cha mguu pamoja na Salim Mbonde ambaye aliumia goti katika mchezo uliopita dhidi ya Mtibwa Sugar.

Kwa mujibu wa mazoezi ya jana, beki Juuko Murshid ndiye atakayecheza nafasi ya Mbonde na Laudit Mavugo atacheza nafasi ya Bocco.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Omog alisema kukosekana kwa wachezaji hao waliokuwepo kwenye kikosi cha kwanza si tatizo kubwa licha ya wao kuwa msaada mkubwa kufanikisha ushindi.

Omog alisema, mara baada ya wachezaji hao kupata majeraha haraka alianza mikakati ya kuwaandaa wachezaji wengine watakaocheza nafasi hizo vizuri.
“Kukosekana kwa Bocco na Mbonde ni pengo kubwa katika timu yangu, kwani ni kati ya wachezaji waliokuwa wanaunda kikosi cha kwanza.

“Lakini kitu kikubwa ninachoshukuru ni kuwa timu yangu ina kikosi kipana cha wachezaji ambao tumewasajili, hivyo tayari nimeandaa wachezaji wengine kucheza nafasi zao.

“Wachezaji hao nisingependa kuwaweka wazi kwa kuwahofia wapinzani wangu Njombe Mji, lakini mashabiki waondoe hofu katika hilo,” alisema Omog.