ASIKUDANGANYE MTU, HAKUNA MWANAMKE/ MWANAUME MBAYA
KILA wiki ninakutana na wewe hapa msomaji wangu. Ni kweli unakutana na mambo mengi. Yapo mazuri na mabaya pia. Lakini huna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kukupa pumzi uliyonayo bila malipo yoyote.
Pia asante msomaji wangu wa XXLove kwa maoni na ushauri ambao umekuwa ukiutoa ili kuboresha jamvi letu hili la kupeana elimu ya uhusiano na maisha kwa jumla.
Miongoni mwa hoja ambazo baadhi ya wanawake zinawakosesha raha, furaha na amani mioyoni mwao, hasa katika upande wa mapenzi ni kuamini kuwa, kuna mwanamke mzuri na mbaya.
Wapo baadhi ya wanawake ambao wamekuwa wakijishuku kuwa inawezekana dhana hiyo ndiyo chanzo cha wao kuachwa na wanaume wanaokuwa nao.
Inawezekana pia kuna mwanamke amewahi kusikia kwa mtu au amekuwa akisimangwa na mpenzi wake kuwa yeye ni mbaya wa sura na maumbile hivyo kumkosesha amani maishani mwake.
Vivyo hivyo, kwa wanaume,
wapo wanaohangaika huku na kule kutaka apate mwanamke mzuri wa maumbile huku akiamini labda aliyenaye ni wa kawaida au si mzuri.
Hii ni dhana ambayo imeziteka fikra za wengi, kwa kuamini kuwa inawezekana aliyenaye si mwanaume au mwanamke mzuri.
Labda msomaji hujui hii, kuwa, hakuna mwanaume au mwanamke mzuri au mbaya. Isipokuwa mwanaume au mwanamke mzuri ni yule ambaye mnaendana, mnaelewana, mnaridhiana na mnaridhishana mnapokuwa faragha.
Ninasema hivyo kwa sababu uzuri ambao unasemwa na kufikiriwa na walio wengi ni uzuri usioweza kusikika, kuhisika, kushikika au kuhadithika.
Mapenzi ni hisia ambayo moyo huitaka kutoka kwa mwanamke au mwanaume husika. Ndiyo maana unaweza kuwa na mpenzi, ukaachana naye kwa mbwembwe nyingi kwa kuamini kuwa si mwanamke au mwanaume anayestahili kuishi na wewe wala mpenzi mwingine yeyote kwa sababu hana uzuri ambao uliufikiria, lakini mwisho wa siku wewe ukaangukia kisogo na mwenzako akafanikiwa kuwa na maisha mazuri ya mapenzi kuliko wewe.
Kuna wakati mwingine unaweza kumuona mpenzi uliyenaye ni mbaya, lakini wakati huohuo kuna mwenzako pale ndiyo kwenye pumziko la moyo wake. Yuko tayari kufanya jambo lolote ilimradi asimuache aende au awe naye.
Wakati mwingine unaweza kuwa unagombana na mpenzi wako kwa sababu tu, hamshabihiani kwa baadhi ya mambo ikiwemo kutokuridhishana.
Inawezekana wewe ni mwanamke ambaye
unamuona mwanaume wako kama siyo mzuri kwa sababu hakuridhishi, vivyo hivyo mwanaume unaweza kuona mke uliyenaye siyo sahihi kwa sababu hujaridhika na jinsi alivyo.
Ukubali au ukatae, lakini ukweli ni kwamba, hakuna mwanamke mbaya, wanawake wote wako sawa isipokuwa inategemea na nini ambacho mwanaume amekipenda na kukielewa zaidi kutoka kwa mwanamke.
Ukitaka kuamini hilo, kuna mwanaume mwingine anaonekana ni mtanashati, lakini mpenzi au mke wake ni mwenye muonekano wa kawaida tu. Lakini ukweli ni kwamba mwanaume huyo inawezekana ameridhika na hali aliyonayo mwenza wake.
Post a Comment