Header Ads

UWANJA WA ARSENAL UMEKUWA SEHEMU YA CHANZO CHA KUVUNJWA STAMFORD BRIDGE




Na Saleh Ally, aliyekuwa London
CHELSEA wanakubali kuwa uwanja wao sasa unatakiwa kufanyiwa mabadiliko, wanataka kuujenga mwingine wa kisasa ambao utakuwa na uwezo wa kuingiza watu 60,000 waliokaa vitini.

Uamuzi huo unafuatia baada ya mafanikio makubwa mfululizo kwa klabu hiyo ya Jiji la London ambayo inaona kweli haistahili kuwa katika Uwanja wa Stamford Bridge, maarufu kama darajani.

Championi limekuwa tena gazeti la kwanza nchini kufika na kufanya ziara katika uwanja huo na kujifunza mambo mengi yanayohusiana na uwanja huo maarufu.

Uwanja huo uko katika Jiji la London katika eneo linalojulikana kwa jina la Fulham, takriban kilomita 20 kutoka ulipo Uwanja wa Emirates unaomilikiwa na Klabu ya Arsenal.

Jiji la London ni kati ya miji maarufu zaidi duniani kati ya miji 1,831 ingawa miji maarufu duniani iko 1,935. Katika Umoja wa Ulaya ambao Uingereza wako katika mchakato wa kujitoa, London inashika nafasi ya pili kwa kuwa na watu wengi ukiwa na wakati wanaokadiriwa kufikia milioni 10 baada ya Paris, Ufaransa ambao una watu milioni 13.5.

Moja ya vitu vinavyoufanya mji huo kuwa maarufu zaidi ni michezo kwa kuwa kuna klabu nyingi zaidi za soka zinazoshiriki Ligi Kuu England ambayo ni ligi maarufu zaidi ya soka duniani.

Kuna Klabu za Arsenal, Chelsea, Tottenham, West Ham, Crystal Palace na Watford na sasa Chelsea imekuwa ikijipanga kufanya kila inavyoweza kuipiku Arsenal kwa thamani ya kifedha.

Kwa sasa, Arsenal ndiyo klabu tajiri na maarufu zaidi katika jiji hilo kwa kuwa ina thamani ya pauni bilioni 1.118 baada ya pato lake kuongezeka kwa asilimia 19 kutokana na mapato. Jambo ambalo limewashawishi Chelsea kuchukua uamuzi wa kuujenga upya uwanja wao wa Stamford Bridge ambao wanaamini ndani ya miaka mitano ijayo utakuwa umekamilika.

Chelsea imebeba makombe matano ya Ligi Kuu England tangu mwaka 2004 Arsenal ilipobeba kombe lake la mwisho. Lakini kwa thamani inaonekana Arsenal iko mbali, kwani thamani ya Chelsea pamoja na kupanda kwa asilimia 38 kutokana na kubeba mataji mfululizo ni pauni milioni 826.

Hii inaifanya Chelsea ione suala la kujenga uwanja halina mjadala ingawa kumekuwa na hofu. Kwani hali inaonyesha Arsenal ilianza kuyumba baada ya kuanza kujenga uwanja. Kuvihimili vyote kwa pamoja, yaani usajili, uendeshaji wa klabu na ujenzi si jambo dogo hata kidogo.
Mmiliki wa Chelsea, Mrusi, Roman Abramovic anaonekana kujipanga kwa hilo ingawa anajua haitakuwa kazi rahisi. Anajua hawezi kuacha kwa kuwa klabu nyingine kubwa ya London ya Tottenham imeanza ujenzi wa uwanja wake wenye uwezo wa kubeba watazamaji 61,000.

Chelsea haiwezi kuacha kuibadilisha Stamford Bridge na ukweli wanastahili kufanya hivyo kwa kuwa katika ziara ya Championi kwenye uwanja huo katika eneo la Fulham, unaonekana umechoka kweli.

Uchovu wa Stamford Bridge si ule ambao utakufanya usikie kero, lakini kwa kuwa gazeti hili lilifika katika viwanja vya Old Trafford jijini Manchester na baadaye Emirates jijini London, Stamford Bridge unaonekana kuwa umechoka kwa maana ya mfumo ambao unaweza kusema hauendani sana na hadhi ya Chelsea.

Unapoingia dimbani, hakuna tofauti kubwa kwa mwonekano na majengo ya viwanja vingine maarufu, lakini uchakavu wa sehemu kadhaa nyuma ya jukwaa pia viti. Lakini utaona hata sehemu kadhaa kama vile chumba cha kupumzikia na kile cha waandishi, kuna tofauti kubwa na viwanja hivyo viwili.

Wataalamu wa sehemu ya historia ya klabu hiyo, wanasema mara kadhaa walilazimika kufanya marekebisho kikiwemo chumba cha kubadilishia nguo ili kuufanya uwanja huo bora kabisa.

Lakini wanakubali, kuwa kama watataka kuendelea kuifanya Chelsea ni yenye hadhi ya juu ni lazima wajenge uwanja mpya na tayari wameomba kuhamia kwenye Dimba la Wembley na wameipata ruhusa hiyo. Tayari kwa sasa uwanja huo unatumiwa na Tottenham ambao si wapinzani wakubwa sana wa Chelsea kama ilivyo kwa Arsenal.

Katika klabu za Ligi Kuu England, tofauti na wengi wanavyodhani, mapato ya mlangoni ni jambo muhimu sana na klabu nyingi zenye viwanja vikubwa zimekuwa zikifaidika sana (hili tutalizungumzia siku chache zijazo).

Ndiyo maana klabu nyingi baada ya kupata umaarufu, zimekuwa zikipambana kuongeza ukubwa wa uwanja. 

Unapoona klabu inapambana kuona timu yake inabeba makombe, usidhani mafanikio hayo ni kwa ajili ya kujionyesha badala yake ni hesabu za kuongeza umaarufu ambao ni kuongeza mashabiki kwa ajili ya kuongeza fedha zinazoingia au faida kwa neno zuri.

Ukiachana na uchakavu wa ndani, Stamford Bridge kwa nje una mvuto zaidi na unaonyesha ni uwanja wa mfanyabiashara kweli maana kuna takriban hoteli nne zilizouzunguka uwanja huo pamoja na migahawa kadhaa.

Hivyo kuwafanya mashabiki wengi kuwa na nafasi ya kuishi katika eneo hilo na pia ni kati ya viwanja vilivyo rahisi kufikika kwa kuwa uko karibu na stesheni ya London Broadway pamoja na vituo kadhaa vya mabasi.

Kwa sasa watu wanaokaa vitini katika Dimba la Stamford Bridge ni 41,631 na kama kweli watafanikiwa kufikisha watu 60,000 kwenye uwanja wao mpya, nafasi ya kuipiku Arsenal ipo lakini lazima wahakikishe wanaendelea kujenga uwanja huku wakifanya kila linalowezekana kushinda  zaidi makombe ya England na Ulaya  zaidi ambayo yamewajengea umaarufu mkubwa. 

No comments