Header Ads

Timu 20 VPL ni mpango mzuri, lakini ‘uswahiba’ wa Toto na Yanga ni tatizo, u-Simba uepukwe


Na Baraka Mbolembole
IKIWA tayari imetangazwa na Shirikisho la Soka Nchini (TFF) kuhusu ongezeko la idadi ya timu shiriki katika ligi kuu ya kandanda Tanzania Bara ni wazi mpango huo umekuja wakati mwafaka ambao kama nchi imekubali kuanza moja. Kuongeza timu 20 kuanziia msimu ujao kutoka timu 16 zinazocheza VPL hivi sasa si jambo jipya, kwani tayari rekodi ya nyuma inaonyesha ligi kuu Bara ilishawahi kuchezwa na timu 24 kwa msimu mmoja.
Baadae  zikapunguzwa timu nne na kusalia 20. Wakati mwaka 2001 timu nne zilizopaswa kuteremka daraja kutoka ligi kuu zilipogoma, Mbanga FC ya Kigoma, Nazarethi ya Njombe, 82 Rangers ya Shinyanga, Singida United ya Singida zilipanda kutoka ligi daraja la kwanza na kuungana na timu 20 zilizokuwa ligi kuu na kutengeza ligi ya makundi mawili yaliyogawanya katika orodha ya timu 12 kwa kila kundi na kucheza ligi kuu mwaka 2002.
Mapenzi haya ya Simba na Yanga yaepukwe
Kugoma kushuka daraja kwa timu nne msimu wa mwaka 2001 kulitokana na uamuzi wa serikali kupitia Waziri wa Michezo ya Utamaduni wakati huo kuingilia mambo ya soka. Waziri wa Michezo na Utamaduni wakati huo aliilazimisha FAT (sasa TFF) kuchezesha ligi ya timu nane bora badala ya Sita bora kama ilivyokuwa imepangwa kabla ya kunza msimu.
Kitendo cha kulazimisha Simba SC kupewa nafasi ya kucheza ligi ya kuamua bingwa wa ligi kuu ‘Sita Bora’ ambayo ilijumuhisha washinda watatu wa juu katika mzunguko wa makundi mawili yaliyogawanywa katika timu kumi-kumi. Hadi  ligi ya makundi inamalizika kwa kila timu kucheza michezo 18 ya nyumbani na ugenini Simba ilikuwa imeangukia katika nafasi ya nne hatua ya makundi, hivyo walipoteza sifa ya kucheza Sita Bora.
Mapenzi binafsi yaliyumbisha msimu mzima na kuleta athari kubwa katika ligi iliyokuwa ikidhaminiwa na Safari Lager (wadhamini wa kwanza wa ligi kuu Tanzania Bara) Simba ilikuwa imeshaporomoka miaka mitano mfululizo ambayo walishuhudia Yanga ikitwaa ubingwa mara tatu mfululizo ( 1996, 1997, 1998)  na Mtibwa Sugar FC ikifanya hivyo mara mbili mfululizo ( 1999, 2000)
Nasema mapenzi binafsi yalivuruga ligi kwa maana walilazimisha ongezeko la timu ambalo halikupaswa kuwepo.
Kanuni ya ligi ilikuwa ikisema timu 3 za juu zitapata nafasi ya kucheza ligi ya sita bora, timu mbili za chini katika kila kundi zitaremka daraja. Wadhamini walifahamu hilo na klabu zilikubaliana hata kabla ya kuanza kwa msimu  lakini baadae Serikali inakuja na kusema ‘haipaswi kuwa sita bora bali chezesheni ligi ya nane bora ili Simba nao wapate nafasi.’
Kuvunjwa kwa kanuni na kuongeza timu kwa amri ya Serikali, FIFA ilichukua hatua haraka sana, Safari Lager hawakusubiri wakajiondoa kudhamini ligi hapohapo na inasemekana Simba ambao walikuja kushinda ubingwa huo baada ya kufanya vizuri katika ligi ya nane Bora hawajawahi kupewa zawadi yao ya fedha kiasi cha milioni 30 zilizokuwa zikitolewa kwa timu bingwa wakati huo.
Kwa TFF (Fat wakati huo) kitendo cha kujiondoa kwa Safari Lager kwao ilikuwa tatizo kubwa. Baadae wakatakiwa kukubali malalamiko ya timu nne ambazo zingepaswa kuteremka kama tu ligi ingechezwa kwa kufuata kanuni za awali.
Timu hizo nne nakumbuka zilitishia kwenda mahakamani kusimamisha ligi ya mwaka 2002 kwa sababu kama Simba haikupata nafasi ya kufuzu Sita Bora na kanuni kubadilishwa baada ya kumalizika kwa ligi, basi hata wao walijiona kuwa na haki ya kubaki ligi kuu kutokana na uvunjwaji wa waziwazi wa kanuni.
Timu 20 tena baada ya kupita miaka 18, nini cha kufanya
Msimu wa kwanza ambao VPL ilikuwa na timu 24 ambazo ziligawanywa katika makundi mawili yaliyokuwa na timu 12 ushindani wa ndani ya uwanja ulikuwa mkubwa mno huku timu kama Tanzania Prisons, Mtibwa zikiongoza timu kutoka mikoani kunogesha ligi.
Ushindani huo ulipelekea kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania Bara kilichoshiriki michuano ya Challenge 2002 mwishoni na kufika fainali kuundwa na wachezaji wengi kutoka nje ya klabu kubwa za Yanga na Simba.
Golikipa, Juma Kaseja alikuwa mchezaji wa Moro United, mlinzi wa kulia Mecky Mexime alifunga nafasi ya Said Sued pale Stars, Dickson Osward, Gerlad Hilu, Lubigisa Madata, Victor Costa, Primus Kasonso, marehemu Christopher Alex,  Ulimboka Mwakingwe, Herry Morris hawa ni baadhi tu ya wachezaji ambao walikuwa nje ya vikosi vya Yanga na Simba na walikuwa katika vikosi vya kwanza vya timu ya Taifa.
Licha ya kuonekana kwa vipaji vingi lakini bado timu kama Bandari Mtwara ilishindwa kuendelea kucheza ligi kutokana na kushindwa kusafiri mwaka 2005 wakati ambao ligi ilikuwa na timu 16. Lakini ni wakati ambao kuliibuka kwa timu kama Moro United na kuungana na timu kama Prisons na Mtibwa Sugar kushindana na timu za Dar es Salaam ambazo historia inawapa kipaumbele zaidi.
Ni mapenzi  yaleyale yaliyowaondoa Safari Lager yakaimaliza Moro United, vigogo wa soka nchini hawakutaka kuona Polisi Moro  FC ikicheza VPL, wala uwepo wa Moro United, wakamaliza nguvu za TP na Mtibwa na hawataki hadi sasa kuona Azam FC ikisimama.
Wadhamini wapo tayari kusaidia
Kuongeza timu nyingine nne kuanzia ligi ya msimu ujao ni wazo zuri lakini hakuna wadhamini ambao wataendelea kubaki  katika vilabu ikiwa wataendelea kuona ‘mapenzi binafsi ya Simba na Yanga’ yakiendesha mpira.
Ukitazama ligi ya msimu huu utaona kuna klabu nyingi zimepata wadhamini wa kuanzia. Mtibwa, Ruvu Shooting, Mbao FC, Stand United, Lipuli FC, Singinda United, Majimaji FC, Ndanda FC, Mbeya City FC, Yanga, Simba, Azam.
Nimezitaja timu hizo 12 lakini ni timu zisizozidi 6 ambazo zimeweza kupata mikata inayoanzia walau miaka miwili huku Simba na Yanga zikiwa na udhamini mkubwa wa miaka isiyopungua minne. Hii inamaanisha nini?
Kwanza, wadhamini ambao walikuwa wakipigiwa kelele na kuombwa kujitokeza sasa wamekuja kutusikiliza watu wa mpira na wameonesha mwamko kuwa wanaweza kusaidia kama watapa ushirikiano. Mikataba yao mifupi kwa baadhi ya timu inamaanisha pia wanajaribu kuona kama kuna nafasi ya wao kusaidia zaidi hapo baadae kama watakuwa wameridhishwa na baadhi ya mambo.
Si kuacha mapenzi katika utawala, ushabiki wa Toto na Yanga umepitwa na wakati
Wakati ule Bandari Mtwara, AFC Arusha, Mji Mpwapwa, Pamba FC zikishindwa kusafiri kwenda kucheza,ligi ilikuwa na mdhamini mmoja tu tena alisaidia zaidi katika vifaa na usafiri kidogo, lakini hata zile timu ‘mama na baba’ wa soka la Tanzania, Yanga na Simba hazikuwa na wadhamini binafsi zaidi ya kutegemea wafadhili ambao nao walikuja kusuasua na pengine kujiondoa katika soka kwa sababu ya ‘mpira kuendeshwa’ kiushabiki zaidi kuliko kusaka maendeleo.
Misimu mitatu iliyopita Toto Africans ilisafiri masaa machache kabla ya mechi yao ya ugenini dhidi ya Kagera Sugar ya Bukoba na hii ilikuja masaa machache baada ya uongozi wa klabu hiyo kusema hadharani hautaweza kuisafirisha timu hiyo kwenda Bukoba.
Juhudi kubwa ilifanywa hadi na klabu nyingine kuhakikisha Toto wanafika Kaitaba Stadium na kucheza vs Kagera vinginevyo walikuwa wakiharibu ligi na kupangua nafasi zote katika ligi iliyochezwa kwa miezi kumi.
Mapenzi yao yanayotajwa kuwepo kati ya Toto na Yanga ndiyo yamekuwa yakiwakimbiza wafadhili  na wadhamini katika timu hiyo hivyo kwa nyakati za sasa ni ngumu timu kushindana inavyotakiwa kwa kutegemea wadhamini wa ligi pekee kwani kuna wachezaji, benchi la ufundi na wafanyakazi wengine klabuni watapaswa kulipwa mishahara hivyo ni lazima timu isake vyanzo zaidi vya mapato,  hapo  ndipo wadhamini wanapohitajika.
TFF  izilinde klabu  ndogo katika sajili
Mbao FC ingeweza kuingiza walau milioni 100 kwa kuuza wachezaji wake mara baada ya kucheza msimu wao wa kwanza katika ligi kuu.  Vipi kuhusu wachezaji wanaosajiliwa na klabu kubwa kutoka Mtibwa Sugar, unadhani Mtibwa ingekuwa na kiasi gani kama Hassan Kessy, Vicent Andrew, Hussein Javu, Said Bahanunzi, Ally Shomari, Mohamed Ibrahim, Shiza Kichuya, Salim Mbonde walisajiliwa Simba na Yanga wangeuzwa walau kwa milioni 15 tu kwa kila mchezaji?
Inawezekana vilabu vya mikoani havijagundua kuwa wachezaji wao vijana wanaweza kuwa sehemu ya chanzo kikuu cha mapato klabuni mwao. Lakini vipo vilavu ambavyo vimejitahidi kutazama hilo lakini inapotokea mchezaji wao kuhitajika na timu kubwa na kuhitaji kiasi Fulani cha pesa hunyimwa. Na baadae mchezaji anahama na kwenda kucheza timunyingine bila TFF kuzisaidia timu ndogo.
TFF inaweza kuzisaidia klabu kwa kuwa somo kuhusu utengenezaji vyanzo vya mapato huku wakiwasisitiza uendelezaji wa vijana ni sehemu ya mradi wa kuingizia klabu mapato. Pia TFF inapaswa kuvisaidia vilabu vidogo pale vinaponyimwa haki zao kuhusu wachezaji waliowalea na kitendo cha kufanya hivyo itakuwa ni kuviongezea kipato vilabu husika, huku pia kuibua vipaji vingine.
Mfano, leo hii Simba wanalalamikiwa kushindwa kuwalipa Moro Youth Soccer Academy kuhusu uhamisho wa Muzamiru Yassin, pia inakwepa kuingia makubaliano na Taasisi hiyo inayoibua wachezaji wengi nchini kuhusu haki ya winga Kichuya.
Kuongeza timu na kuendelea kuvinyima fursa vilabu vidogo hakutaleta faida na kuendelea kuendesha soka kwa mapenzi ya kishabiki na kuacha kanuni itakuwa sawa na kuwaondoa wadhamini wengi ambao tumewaona wakija katika soka hivi sasa lakini hawajaingia ‘mzima mzima.’

No comments