TFF YAAMUA KAMLINDA TSHISHIMBI ASIZINGULIWE
SIKU chache baada ya kiungo mpya wa Yanga, Papy Kabamba Tshishimbi kukumbana na balaa la kuchezewa rafu kibao katika mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Lipuli FC, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeamua kumwekea ulinzi mchezaji huyo.
Katika mechi hiyo ambayo timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1, Tshishimbi alichezewa rafu 11 na wachezaji wa Lipuli huku yeye akicheza rafu mara mbili tu.
Kila wakati wachezaji wa Lipuli walikuwa wakimchezea rafu Tshishimbi ili kumpunguza kasi, jambo lililomfanya kucheza kwa tahadhari kubwa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya TFF, Salum Chama, ameliambia Championi Jumamosi kuwa, wamejipanga kuhakikisha wanakomesha vitendo vya kuchezeana rafu za kukamia na tayari wameshatoa maagizo kwa waamuzi wote wanaochezesha ligi kuu.
Alisema soka ni mchezo wa kiungwana na kila mtu anayeushiriki anapaswa kuwa muungwana na siyo vinginevyo.
“Ligi ndiyo kwanza imeanza na tayari kuna baadhi ya mambo ambayo siyo mazuri yameanza kujitokeza uwanjani, wachezaji kuchezeana rafu za ajabu na za makusudi.
“Tutawaangalia zaidi wachezaji wanaochezewa rafu za makusudi ili kuwapunguza makali, tunataka mchezo wa haki uwanjani.
“Tumejipanga vilivyo kuhakikisha tunakabiliana na kila kitu ambacho hakiendani na kanuni zetu za soka na tumeshazungumza na waamuzi wetu kuhakikisha wanazisimamia vilivyo sheria 17 za soka kama kuna wachezaji ambao hawataki kuzifuata basi wachukuliwe hatua kulingana na kosa alilolifanya uwanjani,” alisema Chama.
Tshishimbi aliwakuna vilivyo mashabiki wa Yanga kwa kiwango safi alichokionyesha akicheza mchezo wake wa kwanza kwenye ardhi ya Bongo dhidi ya Simba katika Ngao ya Jamii, na licha ya Yanga kufungwa kwa mikwaju ya penalti, kiwango cha Mcongo huyo ndicho kilichokuwa gumzo zaidi baada ya mechi.
Katika mchezo wa pili, wapinzani Lipuli walijua kuwa yeye ndiye atakuwa kikwazo kikubwa, hivyo walimdhibiti kwa kumchezea rafu nyingi na kumfanya ashindwe kuwika kama ilivyotarajiwa.
Post a Comment