Header Ads

SAMATTA: MSUVA ANAPITA TU MOROCCO


Simon Msuva.
NAHODHA wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, amemtaja kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Simon Msuva kuwa atafika mbali katika soka la kimataifa kutokana na kufunga mabao ya kiufundi katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Botswana, juzi lakini mwenyewe amesema amekuwa akitembea na Biblia muda wote.
Samatta anayecheza KRC Genk ya Ubelgiji, alisema hayo baada ya mchezo huo wa kirafiki uliochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam ambapo Taifa Stars iliibuka na ushindi wa mabao 2-0, ambayo yote yalifungwa na Msuva.
Msuva aliyejiunga na Klabu ya Difaa El-Jadida ya nchini Morocco kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea Yanga, katika mchezo huo alionekana kucheza tofauti na alivyozoeleka ikiwa ni pamoja na kufunga mabao kwa ufundi wa hali ya juu huku akionyesha utulivu na ukomavu mkubwa.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Samatta alisema kutokana na uwezo alionao mchezaji huyo, anaamini ana muda mchache wa kuitumikia timu hiyo kabla ya kutimkia UIaya kwa kuwa kiwango chake kimekuwa kikipanda kila siku.
Mbwana Samatta.
“Kwa upande wangu bado naona Msuva ni mchezaji mzuri tangu wakati anacheza Yanga, alikuwa akifunga mabao ya kutosha na ndiyo mfungaji bora kwa msimu uliopita, kufunga kwake hakujanishangaza maana nilitegemea kuona hivyo.
“Unajua siku zote nje ni nje, kwa sababu ukiangalia matukio yake ya uwanjani nadhani kuna kitu kimeongezeka, naona nafasi yake ya kucheza Ulaya ipo karibu sana, kama Mungu ataendelea kumsimamia katika kupambana kwake na sitegemei kuona akicheza Morocco kwa muda wote,” alisema Samatta.
Kwa upande wake Msuva, alisema: “Siri ya mafanikio yangu ya kufunga mabao ni juhudi binafsi na kufuata maelekezo ya mwalimu, pia kitabu kitakatifu cha Biblia ninayotembea nayo masaa 24, kinanisaidia kwani naisoma nikiwa kokote hata kambini.
“Lakini kuhamishwa namba na kucheza sehemu ya kati pia kumenisaidia kuwa bora zaidi kwa sababu ni nafasi ambayo naimudu kucheza tangu muda mrefu.”
Ibrahim Mussa na Khadija Mngwai

No comments