Header Ads

POLISI WAFANYA DORIA SINZA KUZUIA MAOMBI YA BAVICHA


Polisi wakiwa kwenye gari (Picha na Maktaba).
Watu wawili wanaosadikiwa kuwa ni wanachama wa Chadema wanashikiliwa na Polisi Mkoa wa Kinondoni kwa kuhojiwa kuhusu mpango wa maombezi uliopangwa kufanyika katika uwanja wa Tip -Sinza, wilayani Ubungo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Murilo Jumanne aliyekuwa uwanjani hapo na kikosi cha askari zaidi ya 25 amesema watu hao walikamatwa saa 3:40 asubuhi wakiwa eneo hilo.

“Tunawashikilia na tutawahoji kama wana uhusiano na kile kilichopangwa kufanyika hapa kwa sababu kilishapigwa marufuku. Kama hawana uhusiano tutawaachia,” amesema Kamanda Jumanne.
Amesema, “Atakayetaka kujaribu aje ila cha moto atakiona kwa sababu jitihada za kuzuia watu wema wasikanyage hapa zimeshafanyika sasa wanakuja kufuata nini.”

Katika eneo hilo, polisi walikuwa wakiziondoa bajaji wakiwataka madereva wasiziegeshe hapo kwa siku ya leo.
Baadhi ya polisi wameonekana wakiwa na mabomu ya kutoa machozi na walifika uwanjani hapo wakiwa kwenye magari aina ya Toyota Land Cruiser.

Uwanjani hapo hivi sasa ni kweupe kukiwa hakuna maandalizi yoyote kuonyesha kuwa patakuwa na maombezi.
Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo –Chadema (Bavicha) jana Jumamosi lilitoa taarifa likisema leo litaungana na viongozi wa kiroho kufanya maombi maalumu kumwombea Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu anayeendelea na matibabu Nairobi, Kenya baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi Septemba 7.
Viongozi wa Bavicha waliofika uwanjani hapo muda si mrefu wamekimbia baada ya polisi kuwafuata walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari.

No comments