Header Ads

MGAHAWA MWEKUNDU WA MAN UNITED UNAVYOINGIZA MAMILIONI KWA SIKU




Na Saleh Ally, Manchester
NIMEFANYA ziara mara kadhaa katika timu mbalimbali zikiwemo zile kubwa kabisa duniani kutoka katika ligi maarufu Ulaya na duniani kote.

Kama unakumbuka nimefanya hivyo Ujerumani nikipata nafasi ya kufika katika Klabu ya Frankfurt na Borussia Dortmund na baadaye Hispania nilipotembelea na kujifunza kupitia Atletico Madrid, FC Barcelona na Real Madrid.

Ninapojifunza inakuwa ni kwa ajili ya wasomaji wa gazeti hili bora la michezo na burudani la Championi, kwa kuwa safari ndefu ya saa zaidi ya 10, mara zote unapotoka Afrika hadi Ulaya, si jambo dogo.



Safari hii nimesafiri kwa takriban saa 24, nikiwa na safari ndefu kutoka Dar es Salaam, Nairobi, Abu Dhabi na baadaye jijini Manchester, England ambako safari nyingine inayonijumuisha mimi na wewe inaanzia hapa.

Nimeanzia katika Klabu ya Manchester United ambako nimepata mwaliko kutoka kwa Klabu ya FC Barcelona ambao wamekuja hapa kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Manchester United, ni mechi ya wakongwe.
Si rahisi nifike hapa na kutojifunza mambo mengi na siku moja kabla ya mechi hiyo iliyochezwa jana, nilifika hadi kwenye Uwanja wa Old Trafford ulio katika eneo la Trafford jijini hapa kujifunza mengi.

Moja ya mambo ambayo yamenifurahisha na huenda mashabiki wa soka wa nyumbani wanaweza kukubaliana nami kuwa ni jambo la kawaida lakini lina ubunifu wa juu kabisa, linaweza kufanyika nyumbani na kuzisaidia klabu zetu mbalimbali kuingiza fedha, ni hili la mgahawa wa Manchester United.



Ndani ya Uwanja wa Old Trafford kuna mgahawa uitwao Red Cafe, kwa Kiswahili ni Mgahawa Mwekundu. Uko katika ghorofa ya tatu ya uwanja huo na zaidi unatumiwa na mashabiki ambao hufika kuutembelea uwanja huo katika sehemu yake ya makumbusho.
Mgahawa huo upo upande wa jukwaa la Alex Ferguson ambalo ndilo jukwaa kubwa zaidi na linaloingiza watu wengi zaidi katika uwanja huo mkubwa zaidi nchini England kwa viwanja vinavyomilikiwa na klabu. Old Trafford inaingiza watazamaji 75,643.

Lakini unatumiwa na mashabiki baadhi wanaokwenda katika mechi zinazochezwa kwenye uwanja huo na nimesema wachache kwa kuwa ni wale ambao tiketi zao huwa ni VIP na tayari wamelipia kupata huduma ya vinywaji na vitafunwa.
Baadhi ya tiketi tayari zinakuwa zimejumlishwa na huduma hiyo na hapo ndiyo utaona uhakika unapoanzia kwa Mgahawa Mwekundu kwa kuwa una uhakika wa kuuza katika kila mechi hata kama baadhi ya mashabiki watakuwa hawajafika, basi fedha huingia ndani ya mgahawa kulingana na idadi ya tiketi zilizokatwa na si wateja wangapi walikwenda kuangalia mechi siku hiyo.

Katika kila mchezo, mgahawa huo unaweza kuingiza hadi pauni 25,000
(zaidi ya Sh milioni 72), jambo ambalo si rahisi hata kwa hoteli kubwa za Tanzania kuingiza robo ya fedha hizo mara moja unapozungumzia huduma ya chakula na vinywaji pekee.



Mmoja wa wahudumu, amesema ingawa si rahisi kujua mahesabu ya kila siku, bila ya kuwa na mechi huingiza hadi pauni 18,000 (zaidi ya Sh milioni 52), mambo yanapokuwa si mazuri sana na kama kipindi cha baridi kali, huingiza pauni 5,000 hadi 8,000 ambacho bado ni kiwango kikubwa cha mauzo kwa migahawa mingine.
Kinachowavutia watu wengi kuingia katika mgahawa huo, kwanza ni kwa kuwa uko katika sehemu maarufu, yaani Uwanja wa Old Trafford ambao una jina kubwa duniani kote.

Ukiwa katika Jiji la Manchester, Old Trafford ni kivutio cha utalii na wengi hasa wageni wanaofika kutoka hapa barani Ulaya, Asia, Afrika na kwingineko duniani, wangependa kufika angalau hata kuuona ‘Live” kwa kuwa wamechoka kuuona mubashara kwenye runinga.
Katika mgahawa huo mwekundu, asilimia 80 ya viti vyake vimebandikwa majina ya wachezaji wa timu hiyo yenye mafanikio zaidi ya ushindi wa vikombe katika Ligi Kuu England.

Viti vina majina ya wachezaji na namba zao. Unaanza na wachezaji walio katika kikosi cha sasa chini ya kocha Jose Mourinho.
Lakini kuna viti vyenye majina ya wachezaji wengi nyota wa zamani kama Rio Ferdinand, Peter Schmeichel, Eric Cantona, Ryan Giggs, David Beckham, Wayne Rooney na wengine kibao.

Mvuto zaidi, unaonekana kwa wengi ni wachezaji walio Man United kwa sasa kama Zlatan Ibrahimovic, Anthony Martial, Marcus Rashford, Romelu Lukaku, Paul Pogba, David de Gea na wengine.
Mashabiki hupenda kuchagua kukaa katika kiti cha mchezaji anayemvutia zaidi. Kama kimepata mtu basi anaweza kuangalia kingine kwa kuwa jina moja linaweza kuwa na viti viwili, vitatu au vinne.



Lakini bado mteja anaweza kuwa na nafasi ya kuchagua mchezaji anayefuatia kwa kumpenda na zaidi na zaidi. Hiyo inakuwa ni katika kujifurahisha.
Kitaalamu inaonyesha mteja hujiona yuko sehemu sahihi na aliyoitaka na wakati mwingine hujiona kama anajumuika na watu anaowapenda kwa kuwa majina yao yamemzunguka, hivyo kumfanya ni mwenye amani na kufurahia zaidi sehemu aliyopo.

Kwa Simba na Yanga zenye mashabiki wengi, jambo hili linaweza kuwa la kujifunza. Kuiga kitu bora na ikiwezekana na kukiboresha zaidi si kitu kibaya. Maana wana wateja lakini hawawaingizii lolote, nimekuwa nikilizungumzia hili mara kwa mara.

Pia hawawatumii wachezaji wao vizuri kuingiza wanachotaka kibiashara.

Huenda hawana watu sahihi wa masoko au hawajajifunza zaidi katika masoko ya soka na wanaweza wakawa wanawapa ushauri katika biashara lakini wasilenge mlango sahihi unaoweza kuwa na faida kupitia soka kama wanavyofanya Manchester United.

Wanaingiza mamilioni ya fedha, hii ni sehemu ya utajiri wao unaowafanya wamsajili wanayemtaka lakini kulipa inavyotakiwa na kuwafanya wachezaji wao kuwa na furaha zaidi, waifanye kazi yao sahihi na kuendelea kuifanya Man United kuwa maarufu na kubwa zaidi.

Karibu jijini Manchester, tuendelee kupeana habari zenye mafunzo.
Tuonane Jumatano.

No comments