MCHAWI WA BONGO MOVIE NI SISI WENYEWE – SHAMSA
NI uwezo wake wa kufanya kweli awapo mbele ya kamera, ndiyo umempa jina na umaarufu mkubwa kunako kiwanda cha kuzalisha filamu za Kibongo. Ni binti mdogo sana kwa uhalisia wa umri, ingawa mwili wake unatoa ishara za kuanza kuingia kwenye ngome ya wahenga.
Wengi wanamtambua kwa jila na Chausiku, lakini wazazi wake walimpa jina la Shamsa huku baba yake akijulikana kwa utambulisho wa Mzee Ford, hivyo si vibaya kama utamtambua kwa nomino ya Shamsa Ford, mama wa mtoto mmoja wa kiume, Terry.
Hivi karibuni mwandishi wetu alifanya mahojiano maalum na muigizaji huyu, nakualika tufuatane sote kweye aya zinazofuata hapa chini, kupata uhondo wa kile alichokisema.
Swali: Kiasili wewe ni mwenyeji wa wapi?
Shamsa: Mimi ni Mzaramo kwa upande wa mama na Mhehe kwa upande wa baba.
Swali: Umezaliwa na kusomea wapi?
Shamsa: Nimezaliwa na kusomea jijini Dar, hadi Kidato cha Nne lakini Kidato cha Tano na Sita nilisomea nchini Uganda ingawa sikubahatika kujiunga na masomo ya chuo kutokana na umasikini wa nyumbani kwetu (sauti ya kunywea kidogo).
Swali: Unaishi na wazazi wako wote?
Shamsa: Hapana, baba yangu alishafariki, alitangulia mbele za haki nikiwa mdogo sana, mwaka 2005, hivyo nimelelewa na mama lakini namshukuru Mungu maana yote ni kwa mapenzi yake.
Swali: Pole sana Shamsa. Vipi, uigizaji ilikuwa ni ndoto yako au ilitokea tu katika kupambana na maisha ili kujihakikishia mkate wa kila siku?
Shamsa: Asante, yeah uigizaji ilikuwa moja ya ndoto zangu tangu nikiwa na umri mdogo kabisa, kwani vituko vyangu viliashiria uigizaji tu, lakini pia nilitaka sana kuwa mwalimu wa wanenguaji (dancers), lakini naona uigizaji ukachukua nafasi kubwa nafsini na kwenye damu.
Swali: Hebu ninong’oneze ukweli, una umri gani?
Shamsa Ford: (kicheko cha aibuaibu), aaah, wewe jamani mimi ni mdogo mno siwezi kutaja miaka yangu hadharani (kicheko tena, awamu hii kwa sauti ya juu). Swali: Ni kitu gani kibaya hutakisahau kwenye maisha ya bongo Movie?
Shamsa: Kuondokewa na wasanii wenzetu, kwa kweli huwa naumia sana kwa sababu huwa naamini waliondoka wakiwa na ndoto nyingi za kutimiza lakini Mungu awapumzishe kwa amani.
Swali: Nani adui namba moja wa tasnia ya Bongo Movie?
Shamsa: (kwa sauti ya haraka sana), ni sisi wasanii wenyewe. Swali: Kivipi? Hebu fafanua tafadhali.
Shamsa: Unajua sisi wasanii tuna asili ya kutopendana, pia tuna wivu wa kutopenda wengine wafanikiwe, yaani ule ubinafsi ni mwingi sana na haitakuja itokee wasanii tukapendana kwa mapenzi ya kweli, sijui na Mungu atusaidie sana.
Swali: Vipi misukosuko ya ndoa, unakabiliana nayo vipi?
Shamsa: Hakuna ndoa isiyokuwa na changamoto kabisa, huo ni uongo lakini ukishaingia kwenye ndoa maana yake unakuwa umeshakomaa kifikra za namna ya kukabiliana na changamoto hizo, jambo la muhimu kwa wanandoa ni kutatua haraka sana migogoro inapotokea kabla ya kuipa nafasi ikakomaa na kuota mizizi lakini pia namshukuru sana Mungu kwa kunipa mume muelewa na mwenye mapenzi ya kweli na mimi.
Swali: Ulizaa na yule mwanaume aitwaye Dickson Matoke, vipi anahusikaje na malezi ya mtoto wenu ingali wewe uko kwenye ndoa na mtu mwingine?
Shamsa: Hana anachomhudumia mtoto, malezi na matunzo yote nayafanya
mwenyewe na mume wangu wa sasa, yeye akitaka kumsalimia mwanaye anawasiliana na mama yangu mzazi, kwa upande wangu hata namba yake sina. Kwa kuwa mara nyingi mwanangu huwa anakaa na bibi yake, basi huwa anawasiliana na mama na kuonana naye huko, lakini ni lazima nipewe taarifa. Swali: Ni tukio gani baya hutalisahau kwa mzazi mwenzako?
mwenyewe na mume wangu wa sasa, yeye akitaka kumsalimia mwanaye anawasiliana na mama yangu mzazi, kwa upande wangu hata namba yake sina. Kwa kuwa mara nyingi mwanangu huwa anakaa na bibi yake, basi huwa anawasiliana na mama na kuonana naye huko, lakini ni lazima nipewe taarifa. Swali: Ni tukio gani baya hutalisahau kwa mzazi mwenzako?
Shamsa: (kwa ukali kidogo huku akimtaja mwandishi kwa jina), aaah, sitaki kukumbuka mambo ya mwanaume yoyote wa nyuma, sitaki kabisa wewe niulize kuhusu mimi na mume wangu wa sasa.
Swali: Lakini tulisikia aliwahi kukushikia bastola usiku wa manane wakati huo mkiishi pale Sinza Madukani, hili lina ukweli gani na ilikuwaje? Hebu eleza kidogo tu. Shamsa: (kimya kidogo na mihemo kwa mbali), sitaki bwana, uliza mambo mengine vinginevyo nitakata simu na nisikupokelee tena.
Swali: Lakini mkikutana mnasalimiana? Shamsa: Dah, jamani! Eeeh tunasalimiana sasa umeridhika?
Swali: Ukiambiwa uwashukuru watu ambao wamekufikisha hapo ulipo kisanaa, utamtaja nani?
Shamsa: Kuna John Lister ambaye ndiye alinichezesha filamu yangu ya kwanza kabisa kuigiza, inaitwa Endless Love, pia kuna JB aliyenichezesha filamu ya Zawadi ya Birth Day, marehemu Kanumba alinipa nafasi kwenye filamu za Saturday Morning na Crazy Love lakini hata Ray alinichezesha filamu ya The Image.
Swali: Ni filamu gani zimekupa jina kubwa? Shamsa: Dah! Ni nyingi lakini Bado Natafuta niliyoigiza na Gabo, Chausiku niliyosimama na Rammy Gallis na hata hizo za Zawadi ya Birth Day na Crazy Love, lakini zaidi Chausiku.
Swali: Ni wasanii gani wa kiume na wa kike unaowakubali hapa Bongo? Shamsa: Nawakubali Gabo, JB, Richie, Steve Nyerere kwa upande wa wanaume na kwa upande mwingine nawahusudu Thea, Monalisa na Riyama Ally, ila nikuambie kitu? Wasanii wote wana umuhimu wao, kila mmoja kwa nafasi yake, ni ngumu sana kusema eti fulani ni wazuri kuliko wengine, hapana.
Swali: Kwa sasa wapenzi na shabiki zako watarajie kazi gani nyingine? Shamsa: Niko njiani kuachia kazi nzuri sana ya Sikujua ambayo nimesimama na Gabo, hivyo wakae mkao wa kula.
Swali: Neno lako la mwisho kwa mashabiki na wadau wa filamu.
Shamsa: Nawapenda sana. Bila wao hakuna Shamsa Ford, waendelee kuniunga mkono kwenye kazi zangu maana kuna wengine waliingiwa na wasiwasi kuona nimeolewa labda nitaacha kuigiza, hapana na mume wangu ananiunga mkono kwenye kazi zangu, nawapenda sana jamani.
Post a Comment