Kikosi cha timu ya Simba SC.

KOCHA Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja ameibuka na kusema mshambuliaji wake mpya, Nicholaus Gyan raia wa Ghana, ni hatari na kuwa kasi yake itaongezeka zaidi pale atakapozoea mazingira kwa kuzoeana na wenzake.


Gyan alifanikiwa kutupia bao lake la kwanza katika timu hiyo kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Hard Rock ya Zanzibar, akiwa amecheza dakika 45 tu za kipindi cha pili ikiwa ni siku chache baada ya kutua Bongo.

Gyan amesajiliwa Simba kwa mkataba wa miaka miwili ya kuitumikia timu hiyo ambapo alitambulishwa rasmi katika Tamasha la Simba Day Agosti 8, mwaka huu kisha alirejea nchini kwao kwa ajili ya kumalizia mkataba wake katika timu aliyokuwa akiichezea.

Akizungumza na Championi Jumatano, Mayanja amesema, kutokana na kiwango ambacho Gyan amekionyesha katika mechi aliyocheza inaonyesha mwelekeo mzuri mara baada ya kuelewana na wenzake kikosini hapo.

“Gyan ni hatari sana, huyu ni mchezaji mzuri kwa jinsi alivyocheza katika mechi ya leo ‘Jumapili’, naamini ataendelea kuwa vizuri zaidi mara baada ya kuzoeana na wenzake.

“Lengo letu msimu huu ni kuona tunafanikiwa kutwaa ubingwa mapema hivyo uwepo wa kikosi kipana kutatusaidia kufanya vizuri zaidi kwenye ligi,” alisema Mayanja.