Header Ads

Katibu wa TFF amefunga biashara Simba na Yanga kucheza Azam Complex


Kaimu Katibu Mkuu wa TFF Wilfred Kidao amezidi kushindilia msumari kwa vilabu vya Simba na Yanga kwenda kucheza kwenye uwanja wa Azam Complex Chamazi ambao ni uwanja wa nyumbani wa Azam FC.
Kidao amesema uwanja wa Azam Complex umechelewa kupewa haki yake ya Simba na Yanga kucheza pale, amehoji kama mechi za CAF zinachezwa Chamazi, Simba na Yanga ni nani wasicheze?
“Azam Complex ni uwanja ambao tayari ulishruhusiwa na shirikisho la soka barani Afrika CAF kuchezewa mechi za kimataifa leo hii ukiwa unauliza kwa nini mechi za Simba na Yanga zipelekwe Chamazi ni jambo la kushangaza.”
“Uwanja wa Azam Complex umechelewa kupewa haki yake lakini kikubwa kuliko yote, watu waliofanya uwekezaji mkubwa namna ile unapowanyima fursa ya kuutumia uwanja wao kwa mechi zote unakuwa hauwatendei haki. Vilevile unawafanya watu wasiwe na tamaa ya kufanya kile kilichofanywa na watu wa Chamazi.”
“Tunataka ligi ya haki, timu ambayo imechagua uwanja wake wa nyumbani basi icheze nyumbani.
“Kwa siku za hivi karibuni mechi za Simba na Yanga zimekuwa zikichezwa kwenye uwanja wa taifa, mechi ambayo inaingiza karibu mashabiki 60,000 uwanjani lakini mechi ijayo ya Simba na Yanga itachezwa uwanja wa Uhuru uwanja ambao unaingiza mashabiki waiozidi 25,000 lakini itachezwa. Kikubwa ni kuhakikisha usalama unakuwepo, tiketi zikiisha hakuna mtu ataeingia uwanjani.”
“Unaposema mechi za Azam dhidi ya Simba na Yanga zichezwe kwenye uwanja wa Taifa unakuwa unazifaifisha hizi timu mbili kwa sababu zinakuwa na mechi nyingi za nyumbani ukilinganisha na Azam.”
“Kwa hiyo wakati mwingine tunapokuwa tunaamua bingwa wa nchi kuna vitu vidogo tunakuwa hatuviangalii lakini vinasababisha bingwa asipatikane kwa haki.”
Kidao ametoa ufafanuzi kuhusu Simba na Yanga kucheza Azam Complex lakini sio viwanja vingine kama Manungu Complex, Mwadui Complex na Mabatini.
“Manungu Complex, Mabatini na Mwadui Complex hatujapeleka mechi za Simba na Yanga kwa sababu ni viwanja ambavyo havina majukwaa. Kwa utafiti tulioufanya tumeona kiusalama itakuwa ni jambo gumu kwa sababu watu wote wanasimama.”
“Kuanzia msimu ujao kama hawatotengeneza majukwaa basi hata mechi za timu ndogo hazitachezwa. Nawaandikia rasmi wajipange kuhakikisha vinaendana na club licencing”.

No comments