Header Ads

Unajifunza nini kutoka Singida United? Mimi tayari wamenipa somo…


August 3, 2017 klabu ya Singida United ilisaini mkataba wa udhamini na kampuni ya YARA Tazania LTD, mkataba wa mwaka mmoja wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 250 za Tanzania na klabu hiyo kufikisha idadi ya wadhamini wanne ambao tayari imewatangaza rasmi (SportPesa, Oryx, Puma na YARA).
Singida United inaendelea kutoa shule kwa vilabu vya Tanzania ambavyo vingi vinadhani wadhamini wanakuja kwa bahati mbaya bila kutumia mipango na nguvu ya ziada kuwatafuta na kuwashawishi kuwekeza kwenye klabu husika.
Kumbuka klabu hii imepanda daraja na bado haijacheza hata mechi moja ya ligi lakini tayari inawadhamini wanne lakini kuna timu zipo kwenye ligi kwa miaka kadhaa na hazina mdhamini hata mmoja lakini bado wamekaa na kunyoosha miguu.
Tumezoea kuona kwamba vilabu vikubwa ndio vinapata wadhamini huenda kutokana na kuwa na mashabiki wengi, lakini kupitia Singida United tunajifunza kitu, wakati mwingine kupata udhamini inategemea na ushawishi, namna gani unakwenda kwa mdhamini na kumwambia aje kwako na atapata nini kutoka kwako (return of investment).
Ukiangalia Singida United utaona wanavyojali wadhamini wao kuonekana, wakiwa wanatambulisha mchezaji au jambo lao lolote rasmi linalohusu klabu, utaona namna wadhamini wao wanavyopata millage ambayo wadau wanaona kuwa kuna watu wapo nyuma ya Singida United.
Kwa hiyo hili linaweza likawa somo kwa vilabu vingine vidogo kwamba kila kitu kinawezekana lakini ni kwa namna gani, hapo ndio unakuja kwa watu waliopewa dhamana ya kuongoza vilabu husika kwamba wana maono kiasi gani ya kuvisaidia vilabu wanavyoviongoza. Singida wanatupa mfano kwamba siku hizi hakuna ujanjaujanja, lazima mambo yaende kwenye mstari kwa sababu dunia imebadilika, mtu anaetaka kuendelea kuishi kizamani atabaki pekeake.
Anachokifanya Festo Sanga na wenzake wa Singida United ndio vitu ambavyo vimekuwa vikihubiriwa miaka nenda rudi, hivi vilabu vinatakiwa kuwa na watu makini wanaojua namna ya kuongoza na kuleta mafanikio kwenye vilabu na mpira wa Tanzania. Wakati Alfred Lucas anazungumzia masuala ya leseni za vilabu wakati wa zoezi la ugawaji vifaa kwa timu za ligi kuu, alisema lazima vilabu viwaajiri watu sahihi kwenye maeneo ya utendaji.
Wakati CAF na FIFA wanaanzisha huo mfumo wa leseni za vilabu walikuwa na maana ya kuona hivi vilabu ni namna gani vinaweza kustawi na kuishi pasipo ujanjaunja kama zamani kwa kuishi vikitegemea kutembeza mabakuli ya michango.
Nitoe pongezi kwa Sanga na Singida United, wanachokifanya kwa mfano na hii kampuni ya YARA (watengenezaji na wasambazaji wa mbolea) ukimsikiliza Sanga utaona sio kwamba wanaenda kwa YARA kwa sababu ya kupewa pesa pekeake. Watu wengi wanakosa wadhamini kwa sababu wakifika wadhamini wanataka pesa kwanza bila kueleza mdhamini atanufaika vipi kutokana na pesa alizotoa.
Kuweka bango pekeake bado haitoshi, lazima watu wabadilike na kufikiria mbali zaidi. Unatakiwa umshawishi mdhamini kwamba akikupa milioni 250 yeye atazirudishaje hizo pesa kupitia timu yako. Ukimsikiliza Sanga yeye alisema, Singida United ni timu inayowakilisha mikoa mitano ya Kanda ya Kati (baadhi ikiwa ni Singida, Tabora, Dodoma, Manyara) hivyo watakuwa ni mawakala wa kusambaza mbolea katika mikoa hiyo.
Kwa nini YARA wasitoe milioni 250 wakati anajua kupitia Singida United watasaidiwa kupata thamani achilia mbali hayo mambo ya millage. Singida United pia wana plan kama klabu inataka kufanya uwekezaji kwenye kilimo na tayari wamenunua mashamba yenye zaidi ya ekari 10,000, kwa hiyo YARA atafanya supply ya mbolea kwao.

No comments