Header Ads

Raia Wa Afrika Kusini Kizimbani Kwa Makosa Manne, Ikiwemo Kutumia Visa Ya Kughushi


RAIA wa AfriKa Kusini, Menolaos Tsampos, (61), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo kujibu mashtaka ya kutishia kwa mtandao, kuishi nchini kwa muda wa miaka minne bila kibali na kutumia paspoti yenye visa ya kugushi.

Mshtakiwa huyo ambaye kabla ya kuanza kusomewa mashitaka yake alitishia kuwapiga waandishi waliokuwa wakimpiga picha kwa kujaribu kurusha mateke na ngumi.

 Amesomewa mashtaka yake hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha ambapo amekana mashtaka yote na amerudishwa rumande hadi hapo upande wa mashtaka utakapothibitisha uhalali wa Visa yake na makazi yake ya kudumu.

Akisoma hati ya Mashtaka wakili wa serikali, Nassoro Katuga amedai, Juni 22, mwaka huu ndani ya jiji la Dar es Salaam, mshtakiwa kwa kutumia mfumo wa kompyuta, alimuandikia barua pepe Costa Gianna Koulos, yenye maneno ya vitisho kwa nia ya kumsababishia Koulos hisia za uoga.

Pia imedaiwa kuwa, Julai 20 Mshtakiwa Tsampos, alimuandikia barua pepe nyingine Koulos yenye maneno hayo ya vitisho na kumpa masaa 48 kumtaka wakae na kumaliza tofauti zao kinyume na hapo atamfanyia kitu kibaya. 

Wakili Katuga ameendelea kudai kuwa mshtakiwa huyo mwenye pasi ya kusafiria namba 246184272,  raia wa Afrika Kusini, Julai 6, mwaka huu alikamatwa akiishi nchini bila ya kuwa na kibali maalumu.

Aidha Agosti 7, mwaka huu katika kituo cha polisi cha Kati, Tsampos, alikutwa akiwa na pasi ya kusafiria yenye namba M00101612 ikiwa na Visa ya kughushi.

Mshtakiwa amekanusha kutenda makosa hayo na amerudishwa rumande baada ya mahakama kuutaka upande wa utetezi kufanya uchunguzi na kuhakikisha kama kweli mshtakiwa anaishi mbezi kama ana visa yake. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 16, mwaka huu.


No comments