NIYONZIMA: HAWA YANGA WATAKUBALI TU
KIUNGO mpya wa Simba, Haruna Niyonzima raia wa Rwanda amesema kuwa mchezo wa Ngao ya Jamii kati yao dhidi ya Yanga utakuwa mgumu na wenye presha kubwa, lakini wanajipanga kuhakikisha wanaibuka na ushindi.
Simba na Yanga zinatarajia kukutana Agosti 23, katika Dimba la Taifa ikiwa ni mchezo wa ufunguzi wa ligi.
Mechi hiyo inatarajia kuwa na upinzani mkubwa hasa ikizingatia timu zote zimefanya maandalizi ya kutosha ambapo kwa sasa Yanga ipo Pemba na Simba ipo Unguja.
Akizungumza na Championi Jumatano, Niyonzima amesema kuwa, mechi hiyo itakuwa ngumu ila wanachotakiwa kukifanya ni kuhakikisha wanafanikiwa kushinda.
“Siku zote mechi ya Simba na Yanga ni kubwa na ngumu na si kwa sababu nipo huku ndiyo niseme hivyo, hata nilivyokuwa Yanga mechi hii tulikuwa tukiichukulia umakini wa hali ya juu.
“Tunahitaji kujipanga ili tuweze kushinda mchezo huu, nimejiandaa vizuri ili niweze kuisaidia timu yangu iweze kushinda,” alisema Niyonzima.
Alimalizia kwa kusema kuwa, kwa sasa anahitaji kutuliza akili yake ili aweze kufanya vizuri katika timu yake mpya kwa kuwa kuhama kutoka timu moja kwenda nyingine kuna presha kubwa.
Post a Comment