BONDIA PIALALI ALIVYOFURAHIA UBINGWA WA GLOBAL TV KUMPA GARI
BONDIA wa ngumi za kulipwa nchini, Idd Pialali ‘Simba Pialali’ amefanikiwa kukabidhiwa zawadi ya gari na Shekhe Omary Ramia wa Bagamoyo mkoani Pwani kufuatia kushinda Ubingwa wa Global Tv, Afrika Mashariki na Kati.
Pialali ni miongoni mwa mabondia watatu wa Tanzania waliopanda ulingoni Julai 23, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Dar Live uliopo Mbagala Zakhem, Dar, kugombania mikanda ya Ubingwa wa Global TV, Afrika Mashariki na Kati ambayo yalirushwa mubashara na kituo cha Global TV Online.
Katika mapambano hayo, Pialali alizichapa na Regin Champion raia wa DR Congo ambaye alimpiga kwa pointi kutoka kwa majaji wote watatu. Mtanzania mwingine, Nasibu Ramadhani ‘Pacman’ alimpiga kwa TKO Yohane Banda wa Malawi huku mkongwe Francis Miyeyusho ‘Chichi Mawe’ akitoka sare na Israel Kamwamba kutoka nchini Malawi.
Licha ya bondia huyo kufanikiwa kushinda katika pambano hilo lakini lile la Pialali lilionekana kuwa bora kwa mabondia wote kutokana na kuonyesha uwezo mkali wa kutupiana makonde katika raundi zote kumi kabla ya majaji watatu kumtangaza bingwa.
“Kwanza napenda kuishukuru Kampuni ya Global Publishers kupitia Global TV ambayo ndiyo walikuwa wadhamini wa pambano langu la ubingwa wa Global Tv, Afrika Mashariki na Kati kwa kuweza kunisogeza sehemu nyingine ambayo sikutegemea kufika.
“Unajua kabla ya lile pambano, niwe mkweli watu wengi walikuwa hawamjui Pialali kwa sababu mapambano yangu mengi nimecheza Kanda ya Bagamoyo na Kiwangwa lakini siyo hapa Dar ambapo ndiyo nyumbani.
“Pambano la ubingwa wa Global TV, Afrika Mashariki na Kati limeweza kunitangaza vizuri na kunifanya nijulikane zaidi hapa Dar na nchi nzima kwa jumla kwa kuwa lilikuwa linarushwa mubashara.
“Kiukweli watu wengi wameweza kujua uwezo wangu ninapokuwa juu ya ulingo hivyo lazima niwashukuru Global TV ambao ndiyo chachu wa mafanikio haya huenda bila yao nisingeweza kuwa bingwa wao.
“Nikwambie kitu, yule bondia niliyepigana naye alikuwa hatari maana sikuwahi kumuona kabla au kuona rekodi zake ila kikubwa nashukuru kwamba nilitumia akili, uzoefu na mbinu nyingi ili kuweza kumshinda.
“Lakini kutokana na uwezo wangu niliamini lazima nitaweza kumshinda mpinzani wangu kwa kuwa yeye alikuwa anatumia nguvu nyingi ndani ya ulingo na mimi nikalazimika kutumia akili nyingi kwa kupiga ngumi ambazo zilikuwa na faida kwa upande wangu.
“Lakini niseme ubingwa wa Global TV siyo wa mwisho kabisa kwangu, malengo yangu ni kuhakikisha nauleta ubingwa wa dunia wa WBC,WBF au WBO nchini kwetu kwani bado nimekuwa nikiendelea kufanya mazoezi makali,” anasema Pialali.
KUHUSU ZAWADI YA GARI
“Kwa sasa sikuwa kabisa na mawazo hata ya kumiliki gari kutokana na hali halisi ya maisha ilivyo ingawa ndoto ya siku moja kumiliki gari nilikuwa nayo ila kwa baadaye sana mambo yatakapokuwa mazuri.
“Lakini pambano la Global TV lilivyonitangaza, kuna watu wengi wameniona hadi kufikia mmoja ya watu ambaye alikuwa mgeni mwalikwa kwa jinsi alivyoona nilivyo kuwa nacheza akawa amevutiwa sana na kazi yangu, anaitwa Shekhe Omary Ramia.
Alishawahi kukuona kabla?
“Hapana hakuwahi kuniona zaidi ya kunisikia tu na siku ile alikuwa amelikwa na Yasini Abdallah ‘Ustaadh’ kwa kuwa ni watu ambao wanafahamiana, baada ya pambano aliniita akanipa simu ya kisasa yenye thamani ya shilingi lakini nane.
“Lakini aliniachia namba yake ya simu kwa sababu aliniambia nimtafute kwani anataka kunipa zawadi nyengine kubwa na kweli muda ulipofika akaniita kunipa zawadi ya gari aina ya Toyota Fielder iwe yangu kabisa kama mwenyewe alivyoniahidi.
“Shekhe Ramia anaishi Bagamoyo na sherehe ilifanyikia huko maana amefurahishwa na uwezo wangu na nidhamu kubwa niliyoionyesha na tupo kwenye mazungumzo ili awe meneja wangu pia amenieleza anataka kunipa kiwanja Bagamoyo na kunijengea nyumba.
“Sasa ndiyo maana nasema lazima niwashukuru Global TV pengine bila yao kuniandalia lile pambano nisingeweza kupata mafanikio haya ambayo leo naweza kuyapata pia namshukuru shekhe kwa moyo wake Mungu amzidishie zaidi kwani sitoweza kumuangusha,” Pialali anasema.
SOURCE: CHAMPIONI.
Post a Comment