MRADI WA UMEME STIEGLER’S GORGE HAUTAATHIRI MAZINGIRA YA PORI LA SELOUS
Katibu Mkuu Mej. Jen. Gaudence S.Milanzi akizungumza na wahitimu wa Mafunzo Maafisa Wanyamapori
KM akisoma kiapo cha wahitimu
Wizara
ya Maliasili na utalii imewataka wadau wa uhifadhi kote nchini kuunga
mkono mpango wa Serikali wa kujenga mradi mkubwa wa uzalishaji wa umeme
katika mto Rufiji kwenye pori la akiba la Selous ambao ukikamilika
unatarajiwa kuzalisha zaidi ya megawati 2,100.
Katibu
Mkuu wizara ya Maliasili na utalii Meja Jenerali Gaudance Milanzi
amesema utekelezaji wa mradi huo wa umeme ni wa muhimu kwa taifa kwani
utasaidia kuharakisha maendeleo ya taifa kuelekea azima yake ya Tanzania
ya viwanda na uchumi wa kati.
Akiongea
wakati akifunga mafunzo ya askari wa wanyamapaori kutoka Mamlaka ya
wanayamapori Tanzania -TAWA na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Katibu
mkuu Meja Jenerali Gudance Milanzi amesema mradi huo wa umeme pamoja na
mradi wa bwawa la maji la Kidunda utachukua eneo dogo tu la pori la
akiba la Selou lenye ukubwa wa zaidi ya kilomita za mraba elfu 50.
Amesema
pori hilo ndilo kubwa miongoni mwa mapori ya aina hiyo ulimwenguni na
ukubwa wake ni zaidi ya nchi za Rwanda na Burundi zikiunganishwa kwa
pamoja.
Katibu
Mkuu amesema ujenzi wa miradi hiyo hauna tafsiri kwamba Tanzania
haithamini masuala ya uhifadhi bali unazingatia uhifadhi wenye manufaa
kwa jamii na maendeleo ya taifa na hasa dhamira ya serikali ya rais Dk
John Pombe Magufuli kuelekea Tanzania ya viwanda ambayo inahitaji
nishati ya umeme itakayoyotosheleza mahitaji ya taifa.
Amesema
Tanzania inatambua umuhimu wa uhifadhi ndiyo maana imetenga eneo la
zaidi ya asilimia 28 ya eneo lote la nchi kavu Tanzania bara kwaajili ya
uhifadhi wa aina mbalimbali ukiwemo wa wanayamapori na misitu ya vyanzo
vya maji ambayo ni muhimu kwa shughuli za kijamii na kiuchumi, “ ni
nchi chache sana duniani zenye eneo kubwa la uhifadhi kama Tanzania”
alisisitiza katibu mkuu.
Katibu
mkuu amewataka wafanyakazi wa wizara na watanzania kwa ujumla kutokuwa
kikwazo kwa utekelezaji wa mradi huo na kwamba wadau wanaotaka kuisaidia
Tanzania wasaidie kuhakikisha inatumia maliasili zake kupiga hatua ya
kimaendeleo ikiwemo misaada ya teknolojia za kisasa na rafiki wa
mazingira kusaidia kufikia malengo yake kimaendeleo.
“Mtakumbuka
mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli
hivi karibuni alipokuwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Pwani amezungumzia
kwa kirefu sana umuhimu wa miradi hiyo ukiwemo wa bwawa la Kidunda na
wa umeme wa Stieglars Gorge, sasa sisi kama wahifadhi na kama watumishi
lazima tumuunge mkono na tusiwe kikwazo katika dhamira hii njema”
alisema Jenerali Milanzi’’.
Ametoa
mfano wa nchi ya Qatar ambayo amesema ilikuwa na eneo la uhifadhi
lililokuwa kwenye orodha ya maeneo ya urithi wa dunia kutokana na uwepo
wa baadhi ya viumbe adimu lakini walipogundua mafuta, waliamua kujitoa
kwenye urithi wa dunia ili wachimbe mafuta na kuinufaisha nchi hiyo na
maendeleo ya wananchi wake.
Akizungumzia
kuhusu tatizo la mifugo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa, Katibu mkuu
amewataka wahifadhi kuhakikisha wanakabiliana na changamoto hiyo na
kusimamia sheria zilizotungwa na Bunge la Jamahuri ya Muungano wa
Tanzania ambazo zinakataza mifugo kuingia hifadhini kinyume cha sheria.
Amesema
ndiyo maana serikali inatumia fedha nyingi kugharamia mafunzo ya askari
wa wanyamapori na wahifadhi ili kuwaongezea ujuzi na weledi wa kulinda
maliasili za taifa kwa kuzingatia sheria zilizopo.
Katibu
Mkuu Meja Jenerali Gaudance Milanzi amezungumzia pia umuhimu wa
kuhakikisha mapori ya uhifadhi yanatumiwa kwa uhifadhi badala ya
kutumika kwa mambo mengine ikiwemo kilimo cha bangi na maficho ya
majambazi na majangili na amewataka wahifadhi na askari kushirikiana na
vyombo vingene vya ulinzi na usalama kuwafichua wahalifu wanaojificha
kwenye mapori hayo na kufanya ujangili na uhalifu mwingine.
Mapema
katika taarifa yake kwa katibu mkuu, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya
Wanyamapori Tanzania -TAWA Martin Loibooki alieleza kuwa mafunzo hayo
yamesaidia kuimarisha uhifadhi kwenye mapori mbalimbali ya akiba nchini
na maeneo ya uhifadhi wa wanyamapori.
Aliwashukuru
wadau mbalimbali wa uhifadhi wa ndani na nje ya nchi wanaofadhili
mafunzo hayo na vitendea kazi juhudi ambazo amesema zimeanza kuzaa
matunda ikiwemo kuongezeka kwa idadi ya tembo na wanyamapori wengine
kwenye mapori mengi nchini.
Katibu
Mkuuakimkabidhi zawadi Afisa wanyamapori wa Kike Bi; Salome G. baada ya
kufanya vizuri mafunzo ya Nadharia na vitendo, wa pili kutoka kushoto
ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu-TAWA
Kaimu Mkurugenzi Mkuu –TAWA Bw. Martin Loibooki akisoma risala mbele ya mgeni Rasmi
katibu
mkuu akiwa kwenye picha ya pamoja na wahitimu wa jinsia ya kike 10 kati
ya 97 waliyohitimu, wa tatu kutoka kushoto waliyokaa ni kaimu
mkurugenzi mkuu-tawa
wahitimu wakitoa heshima mbele ya mgeni rasmi
Post a Comment