Trump amfuta kazi Waziri wa Mambo ya Nje
Rais
Donald Trump amefuta kazi Waziri wa wa Mambo ya Nje, Rex Tillerson na
amemteua Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) Mike Pompeo.
"Mike
Pompeo, ambaye ni mkurugenzi wa CIA, atakuwa waziri wetu wa mambo ya
nje. Atafanya kazi vizuri sana," amesema Trump kwa njia ya Twitter
Jumanne.
"Nakushukuru sana Rex Tillerson kwa huduma uliyoitoa!" ameongeza rais.
Shirika la Habari la CNN limesema nafasi ya Pompeo inatarajiwa kuchukuliwa na Gina Haspel.
Tillerson, Jumatatu alilazimika kukatisha ziara yake ya kwanza ndefu barani Afrika kwa kile kilichoelezwa kwamba kazi nyingi.
“Kutokana
na mahitaji katika ratiba ya waziri, anarudi Marekani mapema baada ya
kukamilisha ziara ya kiserikali Chad na Nigeria,” amesema msaidizi wake
Steve Goldstein.
Tillerson
aliyeanza ziara ya Afrika Jumatano alirudi Marekani baada ya kutembelea
Ethiopia, Djibouti na Kenya ambako ilielezwa aliugua kwa muda.
Kwa
mujibu wa CNN, Trump alimtaka Tillerson kujiuzulu nafasi hiyo tangu
Ijumaa wakati akiwa katika ziara ya nchi kadhaa za Afrika.
Shirika
hilo limemnukuu ofisa mmoja wa utawala akisema Trump alimtaka Tillerson
ajiuzulu ili nafasi hiyo ichukuliwe na mtu mwingine. Ofisa huyo amesema
rais anaona huu ni wakati mwafaka kufanya mabadiliko hasa kutokana na
mazungumzo yanayokuja na Korea Kaskazini na majadiliano mbalimbali
kuhusu biashara.
Muda mfupi baadaye Pompeo alitoa shukrani zake kwa Rais Trump.
“Namshukuru
sana Rais Trump kwa kuniruhusu kuhudumia kama Mkurugenzi wa Shirika la
Ujasusi la CIA na kwa kunipa fursa ya kuwa Waziri wa Mambo ya Nje.
Uongozi wake umeifanya Marekani kuwa salama na natazamia kumwakilisha
yeye na watu wa Marekani katika ulimwengu kwa ajili ya ustawi wa
Marekani.”
Post a Comment