Header Ads

Nape Nnauye: Mungu Aliniokoa na Mdomo wa Bunduki ya Wanyama Wasiopenda Haki Tanzania


Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye amezungumzia tukio la kutishiwa bastola wakati akitaka kuzungumza na waandishi wa habari nje ya Hoteli ya Protea lililotokea baada ya kuachwa katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri.

Katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Nape amekumbushia tukio hilo la Machi 23, 2017 na kuandika, “mwaka mmoja uliopita tarehe kama ya leo Mwenyezi Mungu aliniokoa na mdomo wa bunduki wa wanyama wasiopenda haki! Mungu mkubwa, mbegu ya haki haifi.”

Katika ujumbe huo Nape aliweka picha yake ya video akizungumza na waandishi wa habari nje ya hoteli hiyo kueleza masuala mbalimbali, huku akiwataka vijana kudai haki zao bila woga.

Mtu aliyemtishia bastola Nape alikuwa pamoja na wenzake wawili ambao kwa pamoja walikuwa wakimlazimisha arudi kwenye gari lake na kuondoka, lakini mbunge huyo aligoma na ndipo (mtu huyo) aliporudi nyuma na kuchomoa bastola kutoka kiunoni  kisha kumtishia kabla ya kutulizwa na mwezake.

Baada ya tukio hilo watu hao walitoweka eneo hilo muda mfupi baadaye.

Kufuatia tukio hilo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alisema mtu aliyemtishia bastola Waziri huyo wa zamani wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo hakuwa askari wa Jeshi la Polisi.

Soma: Mwigulu: Aliyemtishia Nape bastola si polisi

Mwigulu alieleza hayo baada ya kufungua mkutano wa kazi wa mwaka wa maofisa waandamizi wa polisi, makamanda wa mikoa na wakuu wa vikosi wa Jeshi la Polisi  uliofanyika mjini Dodoma.

Hata hivyo, Mwigulu alikataa kueleza kwa undani kuhusu mtu huyo kwa kubainisha anatoka taasisi gani wala jina lake.
 
 
Nape Moses Nnauye @Nnauye_Nape
Mwaka mmoja uliopita tarehe kama ya leo Mwemyezi Mungu aliniokoa na mdomo wa bunduki wa wanyama wasiopenda haki! Mungu mkubwa, mbegu ya haki haifi!
 

No comments