Header Ads

OKWI AMPAGAWISHA KOCHA MPYA SIMBA



Emmanuel Okwi
KIKOSI cha Simba,  Alhamisi kilijitanua kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Singida United katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo ambao Simba ilikuwa ikihitaji zaidi matokeo ya ushindi ili ijihakikishie nafasi yake ya kukaa kileleni, ilifanikiwa kupata bao la mapema dakika ya tatu lililofungwa na Shiza Kichuya. Beki wa kati wa timu hiyo,
Asante Kwasi, aliongeza bao la pili dakika ya 24 baada ya kukwepa mtego wa kuotea aliowekewa na mabeki wa Singida United.


Kocha mpya wa Simba, Pierre Lechantre raia wa Ufaransa.
Mara baada ya Kwasi kufunga bao hilo, kocha mpya wa Simba, Pierre Lechantre raia wa Ufaransa, alinyanyuka kwenye kiti chake akiwa jukwaani na kuanza kushangilia pamoja na ofisa habari wa timu hiyo, Haji Manara huku akiwapungia mkono mashabiki wa timu hiyo.

Dakika ya 65 wakati Emmanuel Okwi wa Simba anajiandaa kuingia kuchukua nafasi Mzamiru Yasin, mashabiki wa timu hiyo walikuwa wakimshangilia kwa nguvu jambo ambalo lilimhamasisha straika huyo na kuipatia Simba bao la tatu dakika ya 75.

Okwi aliongeza bao la nne dakika ya 82 ambapo kwa mara nyingine, Mfaransa, Lechantre aliinuka kwenye kiti na kushangilia kwa nguvu. Katika mchezo huo, Simba ilifanya mabadiliko ya wachezaji wawili ambapo ilianza kumtoa Mwinyi Kazimoto dakika ya 22 na nafasi yake kuchukuliwa na Said Ndemla kabla ya dakika ya 65 kutoka Mzamiru na kuingia Okwi.

Kwa upande wa Singida United, dakika ya 59 ilimtoa Kiggy Makasi na nafasi yake kuchukuliwa na Salum Chuku. Kwa matokeo hayo, Simba inaendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 29 ikifuatiwa na Azam yenye pointi 27. Mtibwa Sugar ni ya tatu ina pointi 24, Singida inakamata nafasi ya nne na pointi 23, huku Yanga ikiwa ya tano na pointi 22.
HABARI NA WILBERT LUKONGE

No comments