Header Ads

‘Huwezi kumsifia Rais ukiwa nje ya chama chake’ – Madiwani waliohama CHADEMA kwenda CCM



Chama cha Demokrasia na Maendeleo kimepatwa na pigo lingine kubwa baada ya Madiwani wawili wa chama hicho katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kujiuzulu nyadhifa zao na kuhamia chama tawala cha CCM.

Madiwani hao ni diwani wa Ruaha, Tandesy Sanga mwenzake wa Kwakilosa, Joseph Ryata leo Jumatano Januari 13, 2018 wametangaza uamuzi huo wa kuhamia CCM.
Ryata aliyewahi kuwa naibu Meya wa manispaa hiyo ametangaza uamuzi huo leo alipozungumza na waandishi wa habari, na kuonesha barua aliyoiwasilisha kwa meya na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri Desemba 22,2017.
Ndg Ryata akitaja sababu za kujiuzulu amesema hajaridhishwa na uendeshaji wa Chadema na wa baraza la madiwani la Halmashauri y Manispaa ya Iringa.
Kwa upande mwingine Diwani Sanga amesema uamuzi wake wa kujiuzulu unatokana na kuunga mkono jitihada za maendeleo za Rais Dkt. John Magufuli huku akitaja sababu zilizomfanya aihame CHADEMA kuwa ni tabia ya viongozi wa chama hicho kuwa na nguvu kuliko chama.
Huwezi kumsifia Rais wala utendaji wake ukiwa nje ya chama chake, binafsi nimeshaonywa kwenye vikao hata kutishiwa kuvuliwa uanachama kwa sababu hiyo, kwahiyo bila kutumwa, kushinikizwa wala kununuliwa na yeyote kama inavyodaiwa na baadhi ya watu najiunga na chama kilicho taasisi, si cha mtu mmoja,“amesema Sanga.
Tangu pilika pilika za kuhama vyama zianze mwaka 2017, CHADEMA imeshapoteza madiwani sita akiwemo wa kata ya Kitwiru, Baraka Kimata aliyejiuzulu na kujiunga CCM ambako alishinda tena katika uchaguzi mdogo uliofanyika Novemba 26,2017.
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 CHADEMA ilishinda ubunge wa Iringa Mjini na kupata madiwani katika kata 14 kati ya 18, hivyo kuongoza Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini mwaka 1992.

No comments