Header Ads

Majibu ya Haji Manara kwa Mchambuzi ‘asiyejulikana’


NI HARAAM KUMUUACHIA MTU HUYU!!
Na HAJI S. MANARA
Salaam
Kiasili Haji Manara sio mtu dhaifu anayeweza kukalia kimya shutuma zinazokuja kwake binafsi au taasisi anayoingoza na kuifanyia kazi, ni aina ya mtu anayejua thamani ya habari, anaetaka na kuamini usahihi wa jambo liliopo na linalokuja kwa kadri lilivyo.
Nimeanza na dokezo hilo kusudi ili tuende sawa kwanza, ili kujibu tuhuma na shutuma zinazoelekezwa na baadhi ya magwiji wa ukosoaji nchini hususan kwenye tasnia yetu hii ya kandanda nchini.
Baada ya mkutano wangu na vyombo vya habari hapo jana Jumanne ya tarehe 31-10-2017 pale klabuni Msimbazi, kumetokea wakosoaji wakubwa dhidi yangu binafsi, na wengine wakienda mbali zaidi kwa kunifananisha hata na msemaji wa klabu ya Yanga.
Nianze na hili la maudhui ya mkutano wangu wa jana na wanahabari.
Kwanza niweke wazi kama mtu ninayesimamia idara ya Habari ya klabu, sina mamlaka yoyote ya kuitisha press bila idhini ya uongozi wa klabu ya Simba, na katika hili simjui yoyote afanyae kazi kama yangu mwenye mamlaka ya kuongea na waandishi bila idhini ya uongozi wa taasisi anayoifanyia kazi.
Kwa muktadha huo, press yangu ya jana ina baraka zote za uongozi wa Simba SC na maudhui ya nilichokizungumza jana ni matakwa halali ya uongozi.
Lakini pia niuarifu umma kuwa, bado ninaamini pamoja na wanadaam kutokuwa wakamilifu, waamuzi waliochezesha mchezo wa Jumamosi dhidi ya Yanga na wale waliochezesha michezo mingine niliyoizungumzia jana, kuna makosa waliyafanya na mimi kama msemaji wa klabu, ilikuwa ni wajibu wangu kuzungumzia hilo.
Inawezekana labda kwa baadhi ya watu haikuwa sahihi kwao, lakini dhamira ya klabu ya Simba sio kushutumu, bali ni kutaka ‘fair game’ hatutaki kupendelewa wala kuonewa ndio maana nilitoa TV Set ofisini kwangu na kuileta kwenye ukumbi wa mikutano wa klabu ili kile ninachokiongea kipate legitimacy na sio kuleta porojo za mtaani.
Bahati mbaya sana wale wakosoaji badala ya kujikita na hoja zangu, wakaamua kunishambulia binafsi, na hata walipoamua kujibu hoja waliegemea kishabiki zaidi, huku wakiangalia dhamira za wachezaji bila kuangalia uhalisia wa kisheria na matakwa ya pigo la penati linatolewaje!!
Ndugu zangu mmoja kati ya wachambuzi hao alidiriki kusema huko nyuma, pale tuliponyimwa goli liliofungwa na Laudit Mavugo, siku tulipocheza na Stand United, eti mwamuzi alipitiwa, mtu huyo huyo kwenye maonevu dhidi ya hao hao Stand akasema mfanano wa jezi ndio ulisababisha mwamuzi akosee, lakini kwa mechi ya juzi akasema wachezaji hawakuwa na dhamira ya kushika, sijui kwake yeye dhamira ina tafsiri gani? Unaufuata mpira uliojuu unasema dhamira!!
Lau angekuwa mchambuzi mpya ambae kila uchwao yeye ni kutuhumu na kuishutumu Simba, ningepata tabu, lakini ni yuleyule wa siku zote, na ambae katika kutafuta uungwaji mkono na walio wengi akataka kuhusisha waandishi wote ili kupata ‘moral authority’ na ‘mob support’ toka kwa wanahabari wengine ambao wengi wao tunafanya nao kazi vizuri sana.
Mchambuzi huyu akaenda mbali zaidi kwa kutaka kuonyesha mimi Haji sina ninalofanya klabuni zaidi ya kelele na nimeshindwa hata kuanzisha jarida la klabu.
Katika dunia ya kisasa na inayosoma zaidi mitandao kuliko print media, idara yangu imejikita kwenye magazine za mtandaoni, nadhani anajua kila mwezi tuna jarida maridhawa liliopo kwenye Simba App na ambalo linasomwa na yoyote aliyejiunga na App yetu iliyo na watumiaji wengi kupita App ya klabu yoyote katika ukanda huu wa Afrika.
Yeye mwenyewe bwana mchambuzi anajua kwa nini jarida lake binafsi la michezo lilikufa kifo cha kawaida, utokaji wake ni kama haupo, anatuchuuza klabu kubwa kama Simba ili iingie mkenge.
Nimjibu, Haji ana style yake ya ufanyaji kazi, ana utaratibu wake tofauti na yoyote mwingine, kwangu mimi nakubaliana kabisa na ripoti iliyoonyesha Simba ndio ina followers wengi kwenye pages zote za social media nchini kwa vilabu, anzia kwenye App, Facebook ,Instagram n.k, sasa vipi bwana mchambuzi anataka kufananisha tui na nazi?
Mbali ya hayo, Simba inaongoza kwa kuingiza mapato mengi ya mlangoni kuliko klabu yoyote nchini ndani ya miaka minne ya nyuma ambayo hatukuchukua ubingwa, nimfahamishe jambo hilo halikuja kama uyoga, limetengenezwa na kuandaliwa njia zake makhsuus zilizoifanya tuwe juu.
Nimjuze pia katika dhamana zangu za kiuongozi nimebuni njia za wanasimba wenyewe kujitolea bonus kwa wachezaji pindi timu ikishinda mchezo wa ligi na kombe la Shirikisho, nadhani bwana mchanbuzi hujui kuwa kuna miloni kumi hutolewa kwa kila mchezo ambao Simba hushinda, wanasimba wanajua dhamira na matendo yangu klabuni.
Sio dhamira yangu kujikweza hapa, lakini baadhi ya watu wanaodhani wanaweza kutumia radio wanazopatia mkate kunituhumu na kutaka nionekane mjinga na niwakalie kimya, hiyo kwangu ni big NO.
Na ipo siku tena si nyingi nitawaeleza kwa nini bwana mchambuzi anaichukia sana Simba, ilhali yeye anajinasibu ni mfuasi wa klabu hii kubwa kabisa, ukimchokoza kitange, Ngamia hakuachi, na soon atanipata.
Kwa muda mrefu sana kila uchwao ni kuichokonoa Simba, akidhani atapata huruma ya baadhi yao, Simba hatujasahau toka issue ya Singano, hatujasaha hata tuhuma zako kwa kocha Loga na Kerry, na kwa kuwa wafuasi wa Simba wana ustaarabu wa kutosha hawahangaiki na wewe kama ulivyohangaishwa na wanayanga wakiongozwa na Mzee Akilimali, sentesi hii bwana mchambuzi utakuwa umenielewa sana.
Inafika mahali bwana mchambuzi anazungumzia hata pages zangu binafsi na kusema nataka popularity, ajabu wallah, katika maongezi na andiko lake amekiri mimi ni mtu wa football na nimeanza kitambo uchambuzi wa soka wakati yeye bado yupo kitaani, sasa vipi nitake umaarufu leo? Nina uzoefu mkubwa kabla yake wa kukaa nyuma ya camera, lakini atambue kama popularity ilishatafutwa na wazee wangu waliofanya mambo makubwa kwenye mchezo huu murua zaidi duniani.
Sihitaji hilo kwa sasa, ninalopigania ni maslahi ya Simba na nafahamu sina uadui hata chembe na Yanga, ninao utani nao wa kiasili, ninao upinzani wa dakika 90 na wa jadi, Yanga na Simba si mahasimu ni wapinzani na watani, hilo ulijue mapema bwana mchambuzi wakati huu ukitafuta kuungwa mkono na wanazi wa Yanga.
Mwisho
Niwaombe wanasimba tusikubali kucheza ngoma inayopigwa na watu wa aina hii ambao kwa kila cha Simba ni kibaya na ambao ana dhamira ya kuichafua taswira ya klabu.
Wahindi wana msemo wao, “Deka jahega”. Weka akiba, Ngamia yu macho kuangalia ndege wake, sitahangaika tena na wewe, ila tambua twajua mengi.

No comments