Header Ads

Katika hili Benatia hafichi tabasamu lake kabisa aisee!


Nyota wa kimataifa wa Morocco, Mehdi Benatia amethibitisha kuwa kuiongoza timu yake hio kufuzu kucheza michuano ya Kombe la Dunia nchini Urusi mwakani ni jambo kubwa sana kwenye maisha yake.
Morocco ambao kwa jina la utani hujulikana kama, ‘Simba wa Atlas’, walijikatia tiketi yao kwenye michuano ya Kombe la Dunia 2018, kwa mara ya kwanza tangu walivyofanya hivyo mwaka 1998 baada ya ushindi kutoka kwenye kundi lao.
Benatia, ambae ameshinda mataji akiwa na Bayern Munich na Juventus amesema kufuzu kwa taifa la Morocco ni tukio muhimu sana wakati huu kwenye historia ya maisha yake huku akiongeza kuwa aliwaambia wachezaji wenzake bahati aliyonayo kushinda mataji na Bayern Munich.
“Ni tukio muhimu mno kwa wakati huu kwenye maisha yangu! Niliwaambia wachezaji wanzangu kuwa mimi ni mwenye bahati sana kushinda mataji nikiwa na Bayern na Juve na hii ndio sababu inayotufanya tucheze mpira,” alisema Benatia.
Mlinzi huyo wa Juventus ambae ni moja kati ya walinzi bora kutoka barani Afrika, alikiongoza kikosi cha Morocco kufuzu Kombe la Dunia akiwa kama nahodha wa kikosi hicho.
“Lakini baada ya kujaribu kwa miaka mingi sana kwa ajili ya taifa letu, huku kufuzu kucheza Kombe la Dunia kuna maana nyingi sana kwa upande wangu kama nahodha wa kikosi hiki, hakika ni wasaa mzuri sana kwangu.
“Kila siku nikiamka huwa nakumbuka tukio hili na hapo furaha yangu huanza kujidhihirisha wazi wazi, nina furaha isiyo na kifani, Morocco ni taifa linaloishi mpira, kwa bahati baada ya kuyashuhudia tu mashindano kupitia runinga, sasa na sisi tunakwenda kushiriki,” alimaliza Benatia mwenye miaka 30.

No comments