Header Ads

WANAVYOFANYA MTIBWA KUNA JAMBO LINAWAHUSU LAKINI MNAJIKAUSHA





MTIBWA Sugar imecheza mechi tano bila ya kupoteza hata moja, hali ambayo imeifanya kuongoza Ligi Kuu Bara hadi jana mchana kabla ya Simba kucheza na Stand United mjini Kambarage.

Nimeandika makala haya kabla ya Simba kuivaa Stand United kwa kuwa halikuwa jambo ninalotaka kulizungumzia sana kuhusiana na Mtibwa Sugar.

Sare dhidi ya Yanga, imeifanya Mtibwa Sugar kufikisha pointi 11, ikiwa imeshinda tatu na sare mbili.

Wakati inaibuka na sare hiyo ya bila kufungana na Yanga kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, mjadala mkubwa ulikuwa ni Yanga kupata sare na kutoshinda. Mashabiki wake walikuwa wakilalamika sana.

Yanga hawafurahishwi na matokeo hayo na walichotaka ni kuona Yanga inawachakaza Mtibwa Sugar na kupaa hadi kileleni ili wasubiri mechi ya Simba dhidi ya Stand kwamba mambo yatakuwaje. Mwisho haikuwa wanavyotaka.

Wakati mijadala mingine inaendelea, mimi kidogo nimeangalia tofauti kwamba hata kama ni mwanzoni mwa Ligi Kuu Bara, Mtibwa Sugar inabaki kuwa timu yenye mfumo au mfano wa kuwa shule kwa timu nyingine na huenda kinachofanya wengi tunakichukulia poa lakini ni kikubwa na kinaweza kuwa chachu ya kubadili mambo katika mpira wetu.

Unajua Simba wamefanya usajili wa takribani Sh bilioni 1.3. Watani wao Yanga ukiangalia thamani ya kikosi chao utaona hawako mbali sana. Azam FC ambao waliamua kupunguza thamani ya kikosi, lakini bado hawaondoki katika nafasi ya tatu au ya pili kwa gharama kama utajumlisha wale wachezaji wao wa kigeni walio nao pamoja na makocha na kadhalika.

Lakini Mtibwa Sugar unaijua, timu ambayo kila msimu inauza wachezaji kwa kiasi kikubwa kwenda katika timu nyingine mbalimbali. Msimu unaofuata inaonekana iko katika ubora uleule au zaidi ya ule.

Mtibwa Sugar wanaweza kuuza nyota wake wote wanaotegemewa. Msimu unaofuata wakaibuka na wachezaji usiowajua kabisa, baada ya muda wanakuwa nyota, gumzo na wanatakiwa na timu nyingine ambazo zinaona kama zitawapata basi zina nafasi ya kufanya vema zaidi.

Leo nyota waliokuwa Mtibwa Sugar ambao wapo nje ya kikosi hicho wakiwa na msimu mmoja ni Mohamed Ibrahim, Shiza Kichuya na Mzamiru Yassin. Lakini msimu huu, Simba imemchukua Ally Shomari ambaye ni tegemeo beki ya kulia na kiraka anayeweza kucheza namba zaidi ya nne. Lakini hawa kwa sasa hawaonekani kama ni pengo Mtibwa Sugar.

Badala yake, Mtibwa wakati ikipambana na Yanga, karibu kila aliyeziba pengo la wachezaji hao wanne au zaidi waliondoka likiwemo la kipa Said Mohamed ‘Nduda’ wameonekana ni nyota hasa wenye uwezo wa kuwasumbua au kufanya vizuri hata kuliko nyota wa kigeni wa Yanga ambao wamesajiliwa kwa bei kubwa, wanalipwa mamilioni ya fedha.

Usisahau, Mtibwa Sugar wamekwenda na mwendo wa moja kwa moja usiosita wa kuwatumia makocha wazalendo na wengi wao ni wale walioitumikia timu hiyo wakiwa wachezaji.

Unajua kabla ya Salum Mayanga walikuwepo akina nani, baada yayeye MeckyMaxime, baada ya Maxime unaona anachukua Zubery Katwila na wanaendelea kuwa na mpira unaofanana, unaokwenda kwa utamaduni wa Mtibwa huku wakizalisha wachezaji zaidi wapya.

Tumeona hata wachezaji wakongwe ambao sehemu nyingine walionekana hawafai kama vile wamekwisha na hawana msaada hata kidogo nao wamechukuliwa na Mtibwa Sugar wakarejeshwa katika viwango vyao na kuwa tishio au tegemeo tena.


Umewahi kujiuliza Mtibwa Sugar wanafanyaje? Umewahi kuufikiria ubora huo wa aina yake. Mimi ninawapongeza lakini nawashauri timu nyingine hata Yanga na Simba, pia jifunzeni kwa Mtibwa Sugar huenda mtapunguza gharama fulani na kuongeza ubora zaidi.

No comments