Kocha wa Dodoma FC Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ amesema kuna baadhi ya watu wanamchanganya kocha Joseph Omog ili aonekane hafai kwa sababu ya maslahi yao binafsi, pia amesema anashangazwa kwa nini klabu ya Simba iliamua kuachana na aliyekuwa kocha wao msaidizi Jackson Mayanja. Julio amehoji kwamba, katika mpira ni mahali gani kocha msaidizi anafukuzwa?
“Sisemi kwamba kocha Joseph Omog ni mbaya lakini kuna vitu wanamchanganya ili aonekane hafai kwa sababu kuna watu wana maslahi yao kutaka waonekane wanaijua Simba na kufanya mambo mazuri ambayo hayatusaidii matokeo yake kuna kuwa na malumbano ambayo hayana maana na mwalimu kushindwa kufanya vizuri.”
“Kulikuwa na sababu gani ya kumfukuza Mayanja katika kipindi hiki katikati ya ligi na kumleta mwalimu mwingine msaidizi, nini anachofanya? Kama walikuwa wanataka Omog kwa nini wasimfukuze? Katika mpira kocha msaidizi anafukuzwa vipi? Watu wanakuwa sio wakweli ndio maana tumefika hapa tulipo.”
Julio amesema Yanga sio timu mbovu kama watu wengi wanavyodhani kinachowasumbua wachezaji wa klabu hiyo ni ucho unaotokana na kucheza mechi za ligi na michuano ya kimataifa kwa misimu mitatu mfululizo.
“Kabla ya mechi ya Ngao ya Jamii nilisema tusiwadharau Yanga kwa kuiona ni timu mbovu, Yanga sio mbovu isipokuwa wamechoka, katika miaka mitatu wamecheza pre season moja. Wachezaji wetu hawajitumi kama wenzetu wa Ulaya wanavyojua kujitoa, usifikiri wachezaji wa Ulaya hawanywi pombe wala hawafanyi mapenzi, lakini ligi ikiwa inaendelea wanajua wakati gani wafanye nini.”