Header Ads

LIVERPOOL VS MANCHESTER UNITED; USIENDE NA MATOKEO YAKO MFUKONI, UTASHANGAA





Na Saleh Ally
KOCHA Jose Mourinho ametangaza kumkosa Marouane Fellaini kutokana na kuwa majeruhi lakini akasisitiza atacheza Ander Herrera na kuongeza Manchester United anayecheza anaaminiwa kwa kuwa anapocheza mmoja ni sawa na mwingine kucheza.


Kauli za Mourinho kama zile za “napenda kwenda Anfield, ni sehemu nzuri ya ushindani” kwa kiasi kikubwa anakuwa amelenga kukihamasisha kikosi chake kuwa kazi iliyo mbele yao wanaiweza.


Huenda uhamasishaji wa Mourinho na mwendo wa kikosi cha United, unaruka hadi kuwahamasisha mashabiki wa Manchester United ambao wanaamini hakuna mjadala kwamba leo lazima Liverpool licha ya kuwa kwao “watakaa”.


Rekodi kwa upande wa mechi walizokutana Kocha Jurgen Klopp wa Liverpool na Mourinho katika mechi za ushindani, zinaonyesha Klopp raia wa Ujerumani, ameshinda mechi 3, sare 2 na Mourinho kashinda moja.


Rekodi za Ligi Kuu England tangu makocha hao wachukue timu hizo, zinaonyesha zimeshinda pointi sawa ambazo ni 88 lakini Liverpool imefunga mabao 16 zaidi kwa kuwa imefunga 91 na Man United 75 lakini Liverpool imeruhusu zaidi baada ya kufungwa 54 wakati United imefungwa mabao 31.



Ukiangalia takwimu za makocha hawa wawili, bila shaka utaondoa suala la dharau na kuanza kuamini Manchester United lazima itashinda mchezo huo.

Kuamini “lazima”, hii ni sehemu ya tatizo kubwa lililo mbele kwa kuwa katika soka unaweza kushangazwa. Ninamaanisha hivi, Liverpool inanafasi ya kuishinda Manchester United leo.

Kwa takwimu za Ligi Kuu England, inaonekana kabisa Liverpool licha ya kuwa nyumbani, hawana mwenendo mzuri. Katika msimamo wako nafasi ya saba wakiwa na pointi 12 wakati Manchester United wako nafasi ya pili sawa na Man City wote wana pointi 19.

Katika mechi sita zilizopita, Man United wameshinda mechi tano na sare moja wakati Liverpool wameshinda tatu, sare mbili na kupoteza moja na wamekuwa “wakipigania hali yao” kuhakikisha wanarejea.


Siku nzuri ya Liverpool kurejea ni dhidi ya Man United na wanalijua hilo hata kama Manchester inaonekana kuwa na kikosi bora zaidi.

Wengi wametoa nafasi za kutisha kitakwimu kwa Manchester United, maana hata kwa mchezaji na mchezaji inaonekana wale wa Man United wana nafasi kubwa sana. Kiungo Nemanja Matic anapewa 62% ya kumzuia Coutinho anayeonekana atakuwa na madhara 38%. Dejan Lovren anaonekana ataweza kumzuia Romelu Lukaku kwa 12% na Lukaku anapewa nafasi ya kusababisha madhara kwa 88%.


Kwa takwimu za timu, Liverpool licha ya kuwa nyumbani imepewa 26%, Manchester United 63% na sare ni 11%. Hii inawaongezea uoga mashabiki wa Liverpool na kuwafanya wale wa United waamini wamemaliza kazi.


Hata safu ya ulinzi ya Liverpool, kuruhusu mabao 12 katika mechi saba wakati United wameruhusu mawili tu ni sehemu nyingine ya kuona mambo hayawezekani.


Liverpool itamkosa Sadio Mane ambaye ana nafasi ndogo ya kucheza lakini kumbuka Mohamed Salah na Coutinho wakiwa na Firminho ni hatari, ingawa uchovu barani Afrika na Amerika Kusini pia unaweza kuwapunguza kasi.


Presha kubwa kwa Liverpool ni kwamba wanataka kurudi katika “njia kuu”, Manchester inaonekana gari liko kwenye mteremko na halina breki.



Lakini lazima nyote mkumbuke, mpira wakati mwingine unageuza kila kitu ikiwemo kuzikanyaga takwimu ambazo huwa ni ukweli mtupu.


Liverpool ina wachezaji wanaoweza kubadili matokeo bila mbinu za kocha. Wao wanajua kabisa, kubadilisha “maisha” ya shida wakianzia kwa Man United watakuwa wamezaliwa upya na hawawezi kuacha kufanya kazi kwa juhudi kuzidi kawaida ili wafanikiwe.


Liverpool inazidiwa vitu vingi sana na Manchester United kwa maana ya uhalisia. Lakini kwa maana ya wale wanaotaka mabadiliko, wale wanaotaka kuamka na wanaotaka kupata nguvu mpya, Liverpool ya leo itakuwa nyingine kabisa.


Hivyo kuna uwezekano wa mioyo yenye nia ya kubadilisha mambo ikashinda dhidi ya takwimu madhubuti au kuwashangaza wengi. Kikubwa nasisitiza, dharau mbaya kwa kuwa Liverpool ni timu yenye kila kitu “iliyoteleza”

na inaweza kuamka leo.

No comments