Na Baraka Mbolembole
“Silaha yangu kubwa uwanjani napokabiliana na washambuliaji wa timu pinzani  ni kutumia akili nyingi panapotakiwa, na nguvu panapotumika,” anaanza kusema mlinzi wa kati wa Mbao FC, Yusuph Amos Mgeta nilipofanya naye mahojiano wiki hii akiwa jijini Mwanza wakijiandaa na mchezo wa raundi ya saba katika ligi kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC siku ya Jumamosi ijayo.
Mlinzi huyo mwenye ‘mwili wa beki’ alikuwa wa kwanza msimu huu kuwaonyesha mabeki wa timu  nyingine jinsi ya kumzima mshambulizi wa Simba na kinara wa ufungaji katika VPL, Mganda, Emmanuel Okwi wakati Mbao FC ilipolazimishwa sare ya kufungana 2-2 na Simba SC katika uwanja wa Kirumba, Mwanza mwezi uliopita.
Mgeta ambaye huu ni msimu wake wa pili kucheza ligi kuu, amesajiliwa Mbao FC msimu huu kama mbadala wa Mghana, Ahsante Kwassi aliyejiunga na Lipuli FC ya Iringa msimu huu.
Mgeta alikuwa pacha wa Yusuph Mlipili katika beki ya Toto Africans msimu uliopita ameonekana kucheza vizuri na nahodha wa Mbao, Mrundi, Yusuph Ndikumana katika beki ya kati ya timu hiyo licha ya kwamba tayari wameruhusu magoli 9 katika michezo 6 msimu huu.
Akiwa tayari amecheza michezo minne kati ya sita ya kikosi cha Mbao FC, Mgeta alionyesha namna alivyo na uwezo wa kukimbia na kucheza vizuri na Okwi jambo ambalo lilimuondoa mchezoni mshambulizi huyo wa
Simba aliyefunga magoli 7 katika michezo mitano.
“Tunaenda kucheza na Azam FC na utakuwa mchezo mwingine mgumu. Bado tunapambana kujiweka sawa,” anasema Mgeta ambaye kikosi chake kitawavaa mabingwa hao wa msimu wa 2013/14 kikiwa nafasi ya tisa katika msimamo.
“Kwa sasa naomba uzima tu, nimejipanga kwa nguvu ya mwenyezi Mungu kufanya mambo makubwa msimu huu na kuisaidia klabu yangu.”
MAMBO MENGINE YA MUHIMU KUJUA KUHUSU MGETA
Amezaliwa, Mei 15, 1994 katika Hospitali ya Somanda, Bariadi. Amesoma Somanda Shule ya Msingi, Bariadina kuhitimu darasa la saba mwaka 2006.
Wazazi wake ni wenyeji wa Musoma na kwa sasa wanaishi huko. Baba yake mzazi alikuwa daktari katika Hospitali ya Somanda, Bariadi.
Yusuph ni mtoto wa kwanza kuzaliwa katika familia ya watoto wane ya Mzee Mgeta.
Mlinzi huyo wa kati anavaa jezi namba 16 katika kikosi cha Mbao FC, lakini anasema alichagua namba hiyo kwa sababu alikosa namba anayoipenda-namba 6.
Ni shabiki mkubwa wa mlinzi wa klabu ya Arsenal ya England na timu ya Taifa ya Ufaransa, Laurent Koscielny. Pia ni shasbiki wa mabingwa hao mara 13 wa kihistoria wa EPL.