Header Ads

SUALA LA OMOG, LWANDAMINA LINAVYOONGOZA NA MIJADALA YA MIOYO BADALA YA UHALISIA WA MAMBO





NA SALEH ALLY
SIAMINI kama kila Mtanzania mpenda soka yuko katika mitandao ya kijamii lakini huenda ni sehemu ndogo tu inayoweza kutoa dira kuhusiana na ufahamu wetu kuhusiana na mchezo wa soka.

Katika mitandao ya kijamii, kuna makocha wengi sana ambao wanajua soka hata kuliko makocha wenyewe na bahati mbaya wajuaji hao, hawatoi maoni badala yake hufundisha kupitia huko mitandaoni.

Wataalamu hao wa mitandaoni ambao “wanajua” kuhusiana soka kupitia “ndoto” zao ni watu wanaotoa sababu pungufu, zilizo na ujazo mdogo kueleza hoja zao katika mambo kadhaa ambayo kwangu naona ni vichekesho.

Kwa kuwa wanaotoa hoja hizo mitandaoni ni wanadamu, yaani ni watu kama sisi na tunaishi pamoja basi wanazidi kunichekesha zaidi pale wanapoyatoa hayo ya mitandaoni na kayaingiza mitaa na kufanya wanavyotaka ilimradi tu.

Suala la mashabiki wengi kuanza kupiga kelele kwa makocha George Lwandamina na Joseph Omog wa Simba kuwa wafukuzwe kutokana na matokeo ya timu zao, kidogo inashangaza sana.

Kitu ambacho nakiona ni namna ambavyo mashabiki hao wanashindwa kuwa watu wa takwimu au kuonyesha sababu za msingi, huenda tunapaswa kuamini kwa kuwa ni mashabiki basi wanapaswa kusema chochote.

Dunia imebadilika sana na huenda ni jambo zuri sana kujifunza suala la mahitaji na unachopata kulingana na wakati husika badala ya kupayuka hasa ile tabia ya mashabiki wengi kutaka kusema jambo ili waonekane mbele ya wengine, basi.

Simba imecheza mechi nne, imeshinda mbili na sare mbili. Hayo ni matokeo sawa na yale waliyopata Yanga katika mechi zao nne. Hivyo kila timu katika mechi nne imekusanya pointi nane.

Tofauti ya Yanga na Simba ni mabao ya kufunga na kufungwa. Simba wamefunga mabao 12 na Yanga wamefunga manne. Simba amefungwa mawili idadi hiyohiyo.

Yanga na Simba zinalingana pointi na Prisons ya Mbeya na zinazidiwa na timu moja tu ambayo ni Mtibwa Sugar yenye pointi tisa hii ni kabla ya mchezo wao wa jana dhidi ya Ruvu Shooting. Hizi ni mechi nne tu, kweli ni sawa kusema kocha aondoke kwa sasa?

Inawezekana pia akaondoka ndani ya mechi nne, angalau angekuwa kapoteza mechi tatu mfululizo au zote nne. Lazima kuwe na kipimo sahihi unapozungumzia jambo ambalo linahusisha na kuhitimisha jambo. Bado wanaozungumza hawana takwimu, hawazungumzii takwimu na badala yake ushabiki ili mradi wamesikia na wao wanaendeleza.

Lwandamina wanayetaka aondoke, hakuna wanachojua kinachomkwamisha. Kama wachezaji wanafikia hadi kugoma, maana yake hali ya utulivu ndani ya timu bado haijawa vizuri.

Nashangazwa pia na mashabiki kutojua kwamba, wachezaji wanapokosa mishahara kocha naye anakuwa hajalipwa pamoja na wasaidizi wake, lakini wao waliendelea kufanya kazi zao kwa juhudi kuhakikisha wanakomboa jahazi.

Unataka kocha mzuri zaidi ya Lwandamina, maana yake mshahara wake utakuwa ghali zaidi ya ule anaolipwa Lwandamina kwa sasa. Kumbuka kocha wa sasa amefikia kufanya kazi bila mshahara kwa miezi miwili.

Jaribu kujiuliza, kama kocha huyo anayekuja ataweza kuvumilia, bila mishahara ataweza kufanya kazi. Vipi kama kweli wewe ni shabiki unayeitakia klabu yako mambo mazuri haulii na kuona makocha na wachezaji wanalipwa kwa wakati mwafaka?

Kwa wale wa Simba, wote mnajua kuwa Simba ilisajili wachezaji wapya kikosi kizima. Hii ni mechi ya nne, Omog anafanya kazi ya kuunganisha kikosi upya na ameonyesha inawezekana ingawa imekuwa “mara juu mara chini”, anahitaji kufanya kitu kuweka mambo sawa na huenda ndani ya mechi kadhaa atakaa sawa.

Ukimleta kocha mpya kwa sasa, maana yake anakuja kuunganisha kikosi upya kabisa. Sasa nakuuliza, una uhakika ataweza kuweka mambo sawa haraka au kumpa nafasi Omog angalau hadi mechi ya nane au kumi ili kuwa na jibu. Tukumbuke hakuna kocha aliyepoteza mchezo.


Lwandamina na Omog wanaweza kuondoka lakini tukubali, iwe kwa njia sahihi na si mihemko tu.

No comments