Header Ads

SIMBA YAPANGUA FIRST ELEVEN, KISA MCHEZO WA AZAM


ILI kufanya ushindi uwe mwepesi kwao kwa kila timu wanayokutana nayo, benchi la ufundi la Simba chini ya mkufunzi wake, Joseph Omog raia wa Cameroon limeamua kubadilisha mbinu za kikosi hicho na kutumia nyingine kabisa ili kuwachanganya wapinzani wao, lakini pia wamekipangua kikosi chao cha kwanza.

Awali Simba imekuwa ikitambulika na wapinzani wao kwa kucheza soka la pasi nyingi fupifupi kwa ajili ya kujitengenezea nafasi zake za mabao, lakini kwenye mbinu mpya za kikosi hicho kimeamua kubadilisha mfumo na kutumia pasi ndefu za umbali wa mita 35 hadi 45, kwa ajili ya kusaka mabao yao.

Kwenye mbinu yao hiyo mpya Simba kwa sasa imeamua kumtumia kiungo, Said Ndemla kwa ajili ya kuwa msambazaji mkuu wa pasi hizo ndefu, jukumu ambalo alilifanya vyema kwenye mchezo uliopita mbele ya Hard Rock, ambapo atashirikiana kwa ukaribu na Mghana, James Kotei ambaye naye yupo imara kwenye pasi hizo.

Kuonyesha kuwa kocha wa Simba alinogewa, Demla ambaye amekuwa akipigiwa kelele na mashabiki kuwa anatakiwa kuanza kwenye kikosi cha kwanza, alifunga bao moja na kutengeneza mawili kwa pasi za umbali wa mita 35.

Chanzo makini kutoka ndani ya kikosi hicho kimeliambia Championi Jumatano, kuwa benchi lao la ufundi limeamua kubadilisha mbinu ya pasi fupi kutokana na wengi kuing’amua na aina hiyo ya mbinu imekuwa ikiwapa wakati mgumu kushinda wanapocheza kwenye viwanja vya mikoani ambavyo sio rahisi kucheza aina ya soka wanalolitaka.

“Kwa sasa tumekuja na mbinu mpya kabisa ukiachana na hii iliyozoeleka na wengi ya kutafuta mabao yetu kupitia mipira ya pasi fupi na sasa tumeelekeza nguvu nyingi katika pasi za mbali ambapo aina ya mfumo huu utatubeba pale tutakapokua tunacheza mikoani ambapo mara nyingi hatuna uhakika wa kupata pointi.

“Yaani kwa sasa tunacheza soka la pasi fupi kwa dakika 10 na kama tutashindwa kufunga hata bao moja kwenye dakika hizo basi hapo sasa ndipo tutaanza staili yetu hiyo mpya ya kutumia pasi ndefu na katika mbinu hiyo mpya mikoba ameachiwa Ndemla na Kotei ambapo makocha wameridhishwa na uwezo wao wa kucheza pasi hizo na hivyo Demla ameingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza.

“Kama kwenye mchezo uliopita mbele ya Hard Rock ya Pemba, Ndemla peke yake alipiga pasi tisa ndefu na mbili kati ya hizo zilizalisha mabao na hata Kotei naye hakuwa nyuma kwani alipiga pasi nane za aina hiyo, jambo ambalo linawaaminishia namba wachezaji hao kwenye mfumo huu mpya.

“Lakini pia kuna Mohammed Ibrahim ‘Mo’ na Mwinyi Kazimoto nao wataingia kwenye mfumo huo mpya kwa sababu wameonyesha uwezo katika kucheza aina hiyo ya mbinu na lengo kubwa la kufanya hivyo ni kuhakikisha kuwa tunapata ushindi kwa namna yoyote ile kwenye msimu huu,”kilisema chanzo hicho. 

No comments