Msigwa Ampinga IGP Sirro Sakata la Tundu Lissu Kupigwa Risasi
Mbunge wa Iringa Mjini (CHADEMA) Mchugaji Peter Msigwa amefunguka na kuonyesha kutoridhishwa na kauli ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Nyakoro Sirro kusema Tundu Lissu hakuwahi kutoa taarifa juu ya watu wanaomfuatilia.
Mbunge Msingwa ambaye sasa yupo nchini Kenya kwenye matibabu ya Tundu Lissu ameonyesha kusikitiswa na taarifa hiyo ya IGP ambayo aliitoa Septemba 8, 2017 katika mkutano wa waandishi wa habari na kusema kiongozi huyo hakuwahi kutoa taarifa yoyote polisi juu ya gari ambalo lilikuwa likimfuatilia kabla ya kupatwa na shambulizi hilo la kupigwa risasi.
"Kamanda Sirro Ulitaka Lissu atoe taarifa gani zaidi? Sisi wengine ni wanasiasa, hatuna mafunzo ya kijeshi, Polisi wala Kikachero. Silaha yetu kubwa ni kipaza sauti (microphone), kazi yetu ni kupaza sauti , hoja inapaswa kujibiwa kwa hoja! Siyo kwa mabomu ya machozi, sio kwa virungu na bunduki. Inaonyesha jeshi letu la polisi uwezo wake mkubwa ni kupambana na vyama vya siasa hasa CHADEMA na CUF kuwalinda wakuu wa wilaya na mikoa" aliandika Mchungaji Msigwa
Aidha Msigwa anasema anaumia kuona Tundu Lissu akiteseka kwa ajili ya kutetea haki na Demokrasia ya taifa la Tanzania na kusema alichofanyiwa Tundu Lissu kinampa ujasiri wa kusonga mbele.
"Mungu anakataza kumwaga damu isiyo na hatia! machozi yanitoka kuona rafiki yangu Tundu Lissu akiteseka kwa kutetea haki na demokrasia ya taifa letu, amewakosea nini? Inanipa ujasiri wa kusonga mbele, sitanyamaza, tunakupenda Lissu wewe ndiye shujaa wetu" aliandika Msigwa
Post a Comment