Makala: Kupitia ‘Zilipendwa’ huenda Diamond kamalizana na Lava Lava, Queen Darleen
Ukifuatilia vizuri muziki wa Bongo Flava utagundua kuwa label ya Wasafi Classic Baby (WCB) inayomilikiwa na Diamond Platnumz imekuwa ikifanya vizuri zaidi ukilinganisha na label nyingine.
Ikiwa na miaka miwili sasa imeweza kusimamia wasanii kama Harmonize, Rich Mavoko, Queen Darleen, Rayvanny, Lava Lava pamoja na Diamond mwenyewe. Kitu cha pekee katika lebo hiyo ni ushirikiano mkubwa walionao wa kikazi.
Tuanzie Hapa
Tangu WCB kuanza kusaini wasanii na kuwasimamia, wasanii wanaopata nafasi hiyo wamekuwa katika bahati zaidi ya kufanya kolabo na Diamond akilinganisha na wengine.
Kama kumbukumbu zangu zitakuwa sawa nafikiri AY na Chege ndio wasanii pekee wa Bongo Flava aliyofanya kolabo na Diamond tangu WCB ilipoanza kusaini wasanii.
Hali Ilivyo
Harmonize ndiye msanii wa kwanza kusainiwa na label hiyo na kuweza kutoa wimbo ‘Iyola’ ambao ndio ulimtoa kwa kumtambulisha vema kwenye Bongo Flava.
Wakati bado watu wanahoji juu ya uwezo wa Harmonize huku wakisubiria ngoma yake ya pili kujua uwezo wake, akaamua kumpa shavu bosi wake ‘Diamond’ katika wimbo uitwao Bado ambao ulitoka mwaka jana mwanzoni.
Ngoma hii ilifanya vizuri sana na ninaweza kusema ni wimbo namba moja kwake kwani hakuna wimbo ambao ameutoa na kufikia mafanikio hayo. Njia rahisi kugundua hilo ambayo imekuwa ikitumika zaidi kupima mafanikio ya ngoma ingawa siyo rasmi, ni idadi ya views katika mtandao wa YouTube.
Ngoma ya Bado ina views milioni 16 ambayo ilifuatiwa na ngoma iitwayo Matatizo yenye views milioni 7.4, kisha ‘Niambie’ views milioni 4.7, ‘Show Me’ views milioni 3.1 na Sina views milioni 1.9, hivyo basi wimbo wa Bado aliyofanya na Diamond unabaki kuwa The Best kwake. Weka Nukta hapo.
Baada ya Harmonize kutoka na kujulikana WCB walimsaini Rayvanny ambaye awali alikuwa chini ya usimamizi wa Tip Top Connection. Ngoma yake ya kwanza kutoa ndani ya WCB ilijukana kama ‘Kwetu’ na uliweza kumtoa na kumpa jina kubwa, kisha kuja kufanya vizuri na ngoma ‘Natafuta Kiki’.
Pia naye alipata nafasi ya kutoa wimbo na Diamond lakini haukuwa wake kama ilivyokuwa kwa Harmonize. Wimbo huo uliojulikana kama Salome ulimtangaza sana barani Afrika na ukawa muendelezo wa kufanya vizuri hadi pale aliposhinda tuzo ya BET 2017.
Baada ya Rayvanny alifuatia Rich Mavoko ambaye kabla ya hapo alikuwa anasimamiwa na label ya Kaka Empire kutoka nchini Kenya. Ngoma ya kwanza kutoa ndani ya WCB ni Ibaki Stori ambao ulimrudisha vema katika Bongo Flava.
Kama ilivyokuwa kwa Harmonize, baada ya wimbo wa kwanza naye alimpa shavu Diamond katika ngoma yake ‘Kokoro’ iliyotoka mwishoni mwa mwaka jana.
Kwa mtiriko huo unaona jinsi Diamond alivyokuwa akifanya na kolabo na wasanii kadiri walivyokuwa wakiingia na kukaa katika label yake. Hivyo basi isingekuwa ajabu siku za usoni kusikia kolabo na Queen Darleen au Lava Lava aliyesainiwa mwaka huu.
Zilipendwa Yafunga Kazi
July 19, 2017 Diamond katika ukurasa wake wa Instagram aliandika; “ushawahi waza WCB Wasafi wote kwenye ngoma moja…?”. Ujumbe huu ulihashiria kuwa kuna wimbo wa pamoja wa WCB inakuja ingawa haikufahamika ni lini haswa.
Siku hazingandi na muda unakwenda mbio kama mwaga kwenye chumba cha giza. Hatimaye usiku wa August 25, 2017 Diamond akawapa jibu mashabiki wake kwa kutoa ngoma hiyo ya pamoja ‘Zilipendwa’ ambayo kwa sasa inafanya vizuri kila kona.
Zilipendwa imewakutanisha Diamond, Harmonize, Rayvanny, Rich Mavoko, Lava Lava, Queen Darleen na Maromboso ambaye alikuwa Yamoto Band.
Kama nilivyopambanua katika subtitle ya pili (Hali Ilivyo), Harmonize, Rayvanny na Rich Mavoko walipata nafasi ya kufanya kazi na Diamond baada ya kutoa ngoma zao awali ndani ya WCB.
Karibu katika pointi kuu; Kupitia ngoma ya Zilipendwa Lava Lava na Queen Darleen wamepata nafasi hiyo lakini katika mtindo wa kundi. Je huenda wasanii hawa tusiwasikie katika kolabo na Diamond kama ilivyokuwa kwa wale wa awali? Tusubiri tuone.
Maromboso na Bahati ya Mtende
Huyo ni miongoni mwa wasanii walikuwa wakiunda kundi la Yamoto Band kipindi cha nyuma kabla ya uongozi wa kundi hilo kutoa nafasi ya kila mmoja kufanya muziki wake na kuwa na menejimenti yake.
Hata hivyo mbele ya mashabiki anaonekana ‘kutotumia’ nafasi hiyo kama walivyofanya Aslay na Beka Flavour. Hii ni kwa sababu hajasikika akitoa ngoma ila ukaribu wake na label ya WCB kumeibua madai huenda kuna mipango mikubwa inayoendelea chini kwa chini.
Tumemuona katika tangazo la bidhaa ya Diamond ‘karanga’ na katika behind the scene ya video ya Diamond ‘Eneka’ iliyofanyika nchini Afrika Kusini Maromboso anaonekana akishughulika vilivyo. Tuachane na hilo.
Bahati ya mtende ni pale Maromboso anasikika katika ngoma moja na Diamond wakati bado haijawekwa wazi iwapo amesainiwa WCB bahati ambayo iliwachukua Harmonize, Rayvanny na Rich Mavoko kuipata wakiwa tayari wamedondoka wino.
Post a Comment