Header Ads

Exclusive: Erasto Nyoni kustaafu kucheza Taifa Stars


“Kila zama zina mwisho wake, hakuna marefu yasiyo na ncha” hii ni misemo ya Kiswahili ambayo hutumiwa sana pale jambo au kitu fulani kinapofikia ukomo. Sasa Erasto Nyoni anataka kukamilisha semi hizi kwa kutundika daruga upande wa soka la kimataifa.
 Hamisihemedi.com ilifanikiwa kuzungumza na Nyoni siku moja akiwa kwenye mazoezi ya Stars wakati ikijiandaa kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Botswana mwezi uliopita na hapo ndipo akaweka wazi dhamira yake ya kustaafu kucheza timu ya taifa ‘Taifa Stars’.
“Nimecheza kwa muda mrefu sasa timu ya taifa, imefika wakati inabidi niwapishe vijana waendelee kucheza. Kuna vijana wengi wanaweza kucheza katika nafasi yangu, sitaki kustaafu baada ya mwalimu kuona nimeisha sina nafasi kwenye timu halafu nikaachwa, nataka kuondoka mwenyewe nikiwa bado nina nguvu”-Erasto Nyoni.
“Nimeshawahi kuzungumza na mwalimu kuhusu suala hili, taarifa anazo lakini hatukufikia mwafaka kwa hiyo siwezi kusema ni lini nitatangaza lakini mpango wa kustaafu timu ya taifa upo.”
Erasto Nyoni alicheza mechi yake ya kwanza Stars mwaka 2007, ambapo alifunga pia bao lililoipa ushindi Stars ugenini dhidi ya Burkina Faso mchezo wa kuwania kufuzu kucheza fainali za kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2008.
Mchezaji huyo wa Simba amesema ameweza kudumu kwenye soka kwa muda mrefu kwa sababu anajitunza na kuzingatia misingi aliyojengewa tangu akiwa kwenye academy ya Rolling Stone.
“Nimedumu kwa muda mrefu kwa sababu najitunza, nazingatia mazoezi na kuheshimu misingi ya soka niliyojengewa tangu nikiwa academy.”
Erasto ni miongoni mwa wachezaji 21 walioitwa na kocha Salum Mayanga kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Malawi October 7, 2027.
Kwa sasa ndiye mchezaji aliyedumu kwa muda mrefu zaidi kwenye kikosi cha Stars (zaidi ya miaka 10) na bado ameendelea kucheza kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Salum Mayanga.

No comments