Kati ya makocha ambao walionekana watafukuzwa na timu zao baasi babu Wenger anaongoza, lakini pamoja na kelele zote zilizopigwa na kampeni zote bado Wenger ni kocha wa klabu ya Arsenal.
Lakini sasa hofu kubwa ya kutimuliwa imehamia kwa Carlo Ancelotti, inaonekana wazi kwamba Ancelotti anaweza kuwa kocha mkubwa wa mwanzo kutimuliwa baada ya hali mbaya inayoendelea Bayern Munich.
Kipigo cha jana cha mabao matatu kwa sifuri kutoka kwa PSG kimezidi kukuza habari za Ancelotti kuondoka Bayern Munich huku taarifa zikidai kwamba mchana wa leo mabosi wa Bayern wanakutana kuamua hatma ya Ancelotti.
Suluhu dhidi ya Wolfburg mwishoni mwa wiki iliyopita iliifanya Bayern Munich kuongeza pengo la alama kati yao na vinara wa ligi Borussia Dortmund na sasa mabosi wanaonekana kuchoka.
Tayari watakaochukua nafasi ya Ancelotti wameanza kutajwa huku mlinzi wa zamani wa Bayern Willy Sagnol na kocha wa zamani wa Borussia Dortmund Thomas Tuchel wakipewa nafasi kubwa kuchukua mikoba ya Ancelotti.