Wabunge Waliotimuliwa CUF Watua Mahakamani Leo.......Hakimu Kutoa Uamuzi August 4
Mahakama Kuu ya Tanzania inatarajia kutoa uamuzi wa ama kuyasikiliza au kutoyasikiliza maombi ya Wabunge 8 wa Viti Maalumu wa Chama cha Wananchi CUF waliofutiwa uanachama na Mwenyekiti Prof. Lipumba ifikapo August 4, 2017.
Hatua hiyo imetokana na Wakili wa Serikali Mkuu, Gabriel Malata kuwasilisha pingamizi la awali mbele ya Jaji Lugano Mwandambo akipinga kufunguliwa kwa kesi hiyo.
Malata ambaye anashirikiana na Mawakili wengine Tisa alimueleza Jaji Mwandambo kuwa anapinga maombi hayo kwa kuwa yamefunguliwa kwa njia isiyo sahihi akisema yamefunguliwa bila kuwekwa kifungu sahihi kinachoipa Mahakama mamlaka ya kusikiliza na kutoa uamuzi dhidi ya maombi hayo.
Aidha, amedai maombi hayo yamefunguliwa chini ya kifungu kidogo cha 2(3) ambacho kinaipa mamlaka Mahakama kutumia sheria ya Jumuiya ya Madola.
”Kama maombi hayo yameletwa chini ya kifungu hicho ilipaswa kiwepo kifungu husika kutoka katika sheria ya Jumuiya ya Madola, kisheria kinapaswa kutumika endapo hakutakuwa na sheria yeyote Tanzania inayozungumzia maombi hayo”.Amesema Malata
Malata amedai maombi hayo ni batili, hivyo yatupiliwe mbali kwani hata Mahakama iliwahi kutoa uamuzi dhidi ya kifungu hicho.
Post a Comment