Header Ads

Vodacom imegawa vifaa vya milioni 500 kwa timu za VPL


Wadhamini wa ligi kuu Tanzania bara kampuni ya Vodacom Tanzania imekabidhi vifaa mbalimbali kwa timu zitakazoshiriki VPL msimu ujao 2017/2018 ikiwa ni pamoja na jezi za mazoezi na zile za mechi.
Vifaa vyote vilivyokabidhiwa kwa timu 16 zitakazocheza VPL msimu ujao vina thamani ya shilingi milioni 500 za Tanzania.
Mkurugenzi wa idara ya masoko na usamazaji Vodacom Bw. Hisham Hendi amesema, katika kuhakikisha ligi ya Tanzania bara inaendelea kuchezwa vizuri, Vodacom wanakabidhi vifaa mbalimbali kwa timu shiriki ikiwa ni jezi za mazoezi na mechi, viatu vya mazoezi na mechi, substitution boards, vibendera, jezi za waamuzi pamoja na vifaa vingine vinavyohitajika.
“Tunafurahi kukabidhi vifaa hivi ikiwa ni utekelezaji wa matakwa ya udhamini, tunaamini timu zitakazoshiriki ligi kuu Tanzania bara zimejiandaa vizuri kwa ajili ya msimu mpya utakaoanza hivi karibuni.”
Hendi amesema Vodacom itaendela kudhamini ligi kuu kwa sababu mchezo wa soka unapendwa na watu wengi huku wao wakitaka kuhakikisha watu wengi wanapata burudani kutoka kwenye mchezo waupendao huku wengi kati ya hao wakiwa ni wateja wao.
Amesema pia Vodacom wanaamini michezo ni ajira na ikiendelezwa watu wengi wanaweza kunufaika, serikali pia inaweza kupata mapato kupitia kodi itakayopatikana katika sekta hii.
Hendi amewaomba wadhamini wengine kujitokeza na kudhamini ligi kuu ili kuiongezea thamani ambapo wachezaji watanufaika pia: “Tukiunganisha nguvu, tutapata wachezaji wengi wataoenda kucheza kimataifa. Wadhamini waendelee kujitokeza pia katika kudhamini soka la vijana ili kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vyao.”
Kwa upande wa bodi ya ligi, afisa mtendaji mkuu Bw. Boniface Wambura ameishukuru kampuni ya Vodacom kwa kuendelea kuwa wadhamini wa ligi pia amevitaka vilabu kuheshimu nembo ya mdhamini kipindi chote cha ligi.

No comments