POLISI DAR WAMNASA MUUZAJI WA MISHIKAKI YA PAKA
HATARI! Njemba mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Sadiki, ambaye ni muuza mishikaki katika eneo lililo karibu na jengo la Kibo Complex, Tegeta jijini Dar amenaswa na polisi kwa tuhuma za kukutwa akiuza mishkaki ya paka.
Chanzo chetu cha habari kilidai kuwa walaji wengi wa mishkaki ya Sadiki wamekuwa wakipatwa na shaka na nyama hiyo kutokana na ladha yake kuwa tofauti, lakini kila mara wakiuliza kuhusu jambo hilo, jamaa huyo amekuwa akiwatoa wasiwasi kwa kuwaambia kuwa kitoweo hicho ni cha ng’ombe.
“Kuna siku mteja mmoja alipomuuliza Sadiki kama mishkaki ni mnyama gani jamaa alimsisitizia kuwa ilikuwa ni nyama ya ng’ombe isiyo na mashaka ambapo mteja huyo alishindwa kuendelea nayo na kuiacha bila kudai pesa,” kilisema chanzo hicho.
Imedaiwa kutokana na shaka ya wateja wa mishkaki hiyo inayoletwa na ladha isiyo ya kawaida ya nyama, ambayo pia hunogeshwa kwa viungo vya aina mbalimbali, wananchi wa eneo hilo waliamua kumuwekea mtego ili kubaini ukweli.
Alhamisi iliyopita, wakati akiwasili katika kijiwe chake kuendelea na kazi yake ya kuuza mishikaki, ghafla wananchi walimvamia na kumnyang’anya ndoo yake ya nyama na kuifungua, ndipo zilipokutwa nyama hizo zilizodaiwa kuwa za paka.
Wananchi wenye jazba baada ya kuona hivyo walitaka kumuangushia kipigo, lakini walitokea polisi wa doria ambao walimuokoa mfanyabiashara huyo na kwenda naye kituoni kumhoji zaidi kuhusiana na tuhuma hizo.
Gazeti la Uwazi lilimpigia simu Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP, Jumanne Muliro kumuuliza kama anazo taarifa hizo, na kueleza kinachoendelea ambapo kamanda huyo alisema askari wake bado hawajamfikishia taarifa hizo na kusema huenda kuna mambo walikuwa wakiendelea kuyaweka sawa ili wamfikishie habari iliyokamilika.
“Ninafuatilia suala hilo na nitakupa majibu,” alisema, lakini mpaka tunaelekea mitamboni alikuwa bado hajarudisha majibu.
Post a Comment