Header Ads

Misimu minne ambayo bingwa VPL alipaswa kutoka nje ya Dar


Na Baraka Mbolembole
MSIMU wa 54 wa ligi kuu Tanzania Bara unataraji kuanza Jumamosi hii kwa mipambano 7 kuchezwa katika viwanja tofauti nchini. Simba SC itakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting katika uwanja wa Taifa, mabingwa mara mbili wa zamani Mtibwa Sugar FC watakuwa nyumbani Manungu Complex kuwavaa Stand United.
Mabingwa wa msimu wa 2013/14 timu ya Azam FC itakuwa Nang’wanda Stadium kusaka ushindi wa kwanza katika uwanja huo dhidi ya wenyeji wao Ndanda FC. Huko mjini Njombe wanataraji kushuhudia mchezo wa kwanza wa ligi kuu baada ya kupita miaka 16 wakati wenyeji na timu mpya kabisa katika ligi hiyo Mji Njombe FC itakapowakabili mabingwa wa zamani wa Tanzania, timu ya Tanzania Prisons ya Mbeya.
Mchezo mwingine unaotazamwa sana Jumamosi hii ni ule utakaowakutanisha wenyeji Mwadui FC dhidi ya Singida United ambao wamerejea VPL msimu huu baada ya kushuka miaka 15 iliyopita. Kinachofanya mchezo huo kufuatiliwa sana ni kutokana na sajili ghali zilizofanywa na timu hiyo kutoka Mkoani Singida ukiongozwa na ujio wa kocha mshindi mara mbili wa VPL, Mholland, Hans van der Pluijm.
Mchezo mwingine leo Jumamosi unataraji kupigwa katika uwanja wa Sokoine, Mbeya wakati wenyeji Mbeya City FC itakapowakaribisha Majimaji FC kutoka Songea, Kagera Sugar FC ambao walimaliza nafasi ya tatu msimu uliopita wataanza msimu kwa kuwakaribisha Mbao FC katika uwanja wa Kaitaba.
Baada ya mipambano hiyo saba ya leo, mabingwa watetezi Yanga SC wataanza kampeni yao ya kushinda ubingwa wa nne mfululizo kwa kuwavaa Lipuli FC kutoka Iringa timu ambayo imerejea VPL baada ya kushuka takribani miaka 16 iliyopita.
Kuelekea msimu huu mpya wa VPL nakukumbusha misimu minne ya zamani ambayo ilishuhudiwa timu za Prisons mara mbili, Moro United, na Mbeya City FC jinsi zilivyoshindwa kutwaa taji hilo kati ya mwaka 2002 haei 2013/2014 wakati wanasoka wengi walipoamini timu hizo zinaweza kushinda ubingwa.
Kumbukumbu hizi ni kama onyo na funzo kwa timu nyingine za mikoani ambazo zinaaminika haziwezi kushinda ubingwa huo mbele ya timu za Dar es Salaam (Yanga, Simba na Azam FC) Kuna sababu nyingi za nje ya uwanja ambazo ziliwaangusha Prisons, Moro na Mbeya City kushinda ubingwa wakati ambao walikuwa wakikidhi ubora huo misimu iliyopita.
2002
Yanga ilitwaa ubingwa kwa stahili ya kuvutia siku ya mwisho ya msimu katika uwanja wa Sokoine baada ya ‘kuichakaza’ Prisons magoli 4-1. Mmoja kati ya wachezaji waliokuwepo katika kikosi kabambe cha Prisons msimu huo nilipata kukutana nae miaka 6 baadae katika harakati hizi za soka pale Morogoro na akanieleza mambo ya kukatisha tamaa.
Kuelekea mchezo huo wa mwisho wa msimu Prisons ilikuwa inahitaji sare tu dhidi ya Yanga ili kushinda ubingwa, lakini kilichokuja kutokea ni mambo ambayo watu wa Mbeya hawapendi kuyakumbuka.
“Naamini mechi ile tulifungwa kwa sababu kocha wetu alitaka Yanga ichukue ubingwa.” ni sehemu ya maneno ya mchezaji huyo wa zamani wa Prisons wakati tulipokutana katika timu ya Bukina Faso FC ya Morogoro mwaka 2008.
Aliyekuwa kocha wa Prisons wakati huo alipanga kikosi tofauti na kilichozoeleka huku akiwaacha benchi wachezaji wake 6 wa kikosi cha kwanza. ” Huwezi kuamini kocha wetu alikutwa chooni akishangili.”
Msimu huo Prisons ilikuwa na kikosi bora kabisa kikiongozwa na mlinda mlango, Dennis Edwin, Gerlad Hilu, Seka Bugoya, Samson Mwamanda, Victor Kilowoko, Osward Morris, Primus Kasonso, Herry Morris, Geofrey Bonny na wengine wengi waliokuwa na ubora iliangushwa na mapenzi binafsi na ushabiki wa aliyekuwa kocha wao mkuu wakati huo ambaye ni ‘mtu hasa wa Yanga.’
2005
Wakati Prisons iliangushwa na mapenzi binafsi ya aliyekuwa kocha wao mwaka 2002, Mkenya, James Siang’a yeye alimalizwa vibaya na baadhi ya wachezaji wake muhimu na alipokuja kustuka tayari alikuwa ameshachelewa sana na kushuhudia kikosi chake cha Moro United kikiwapisha Yanga na kushinda ubingwa uliokuwa mikononi mwao kwa robo tatu ya msimu.
Moro United kwa nguvu ya aliyekuwa mmiliki wa vituo vya mafuta ilikusanya kikosi kikali msimu wa 2005 huku ikiwasajili wachezaji muhimu kutoka Yanga kama Wacongoman, Pitchou Kongo, Patrick Katalay, Wazir Mahadhi, Salum Sued, na kushinda vita nyingine ya kuwasaini wachezaji nyota wakati huo golikipa, Ivo Mapunda, mlinzi wa kulia Shadrack Nsajigwa usajili wa wachezaji hao ulifanya timu hiyo kuwa maarufu sana Afrikb Mashariki.
Si tu kilikuwa kikosi bora katika makaratasi lakini ukweli timu hiyo ilionesha kandanda la hali ya juu. Kiungo mlinzi Faustino Lukoo, wings Julius Mrope, Nsa Job ni baadhi ya wachezaji wengine mahiri waliokuwepo kikosini humo.
‘Chelsea ya Bongo’ kama ilivyokuwa ikifahamika ilimaliza mzunguko wa kwanza wa mechi 15 katika ligi iliyokuwa na timu 16 pasipo kupoteza mchezo. Moro ilikuwa kileleni kwa tofauti ya alama 11 baada ya ushindi 15 mfululizo katika mzunguko wa kwanza.
Wengi waliamini timu hiyo ingetwaa ubingwa na kwa huduma ambazo niliona wakati fulani wakipatiwa wachezaji wa timu hiyo hata upande wangu niliamini timu hiyo ilikuwa ikienda kushinda ubingwa wake wa kwanza wa ligi kuu.
Lakini kilichokuja kutokea mzunguko wa pili ni habari mbaya ambayo ilimuondoa moja kwa moja katika soka aliyekuwa mmiliki wa timu hiyo, M.Balhabou. Katika michezo 15 ya raundi ya pili timu hiyo ilishindwa kukusanya alama walau 15 ambazo zingewapa ubingwa mbele ya Yanga iliyomaliza na pointi 59.
Iliumiza sana kwa wakazi wa mkoa wa Moro ambao waliamini timu hiyo ingekuwa ya tatu kutoka mkoani humo kushinda VPL baada ya Mseto SC (1975) na Mtibwa Sugar FC iliyoshinda mara mbili mfululizo (1999 na 2000).
Wakati ligi ikiendelea huku timu ikishindwa kupata ushindi katika michezo dhidi ya timu zote walizofunga katika mzunguko wa kwanza, zikaanza kuzuka taarifa za chinichini kuwa kuna baadhi ya wachezaji wanafungisha makusudi kwa kuwa wamepewa ahadi na bonasi ya kusajiliwa na timu fulani kubwa ikiwa watahakikisha Moro United inaanguka.
Ilikuwa ni ngumu kujua lakini vipigo vya 1-0, 1-0 vilikuwa vikishangaza sana kwa sababu timu ilikuwa ikitawala michezo yao. Ikatazamwa vizuri na kuonekana kuna wachezaji wa idara zote muhimu wanashirikiana.
Na kilichokuwa kikifanyika wanaruhusu goli kasha wanacheza soka maridadi sana. Moro walipokuja kustuka Yanga walikuwa kando yao na presha ikawashinda wakakosa taji. Baada ya msimu kumalizika ukiwatoa Jumanne Ramadhani, Lukoo, wachezaji wanne wa safu ya ulinzi walisajiliwa Yanga (Ivo, Nsajigwa, Lulanga Mapunda, Mahadhi) huku Sued akienda zake Mtibwa.
2007/08
Baada ya kushindwa siku ya mwisho ya msimu kuisaidia Prisons kushinda VPL mwaka 2003, kocha Juma Mwambusi alishuhudia akipoteza nafasi nyingine ya uongozi wa alama 9 na kuwapisha Yanga wakishinda ubingwa mbele ya Prisons msimu wa kwanza wa kalenda ya Agosti-Mei.
Mwambusi alitengeneza kikosi imara kwa kuwategemea zaidi wachezaji wenye asili ya Mbeya huku uwezo wa viungo wake mahiri kama Misango Magae ‘Diego wa Mbeya’ G.Boony (mwenyezi Mungu amrehemu) ukifanya timu hiyo kutingisha sana msimu wa 2007/08.
Baada ya kushindwa kwao mwaka 2002, kushindwa kwa Moro United mwaka 2005, msimu huu ulikuwa wazi kwa klabu za mikoani kushinda VPL lakini nafasi hiyo ya wazi ilipotezwa na kikosi cha Mwambusi na baadaye kukazuka habari zilezile kuwa ‘timu hiyo ilihujumiwa’ kutokana na mapenzi binafsi ya baadhi ya watu huku jina la Yanga likitajwa kwa mara nyingine.
2013/14
Ndiyo tulipata bingwa mpya msimu huu lakini bingwa aliyekidhi ubora alipaswa kutoka nje ya Dar es Salaam, na Mbeya City FC ilipaswa kuweka rekodi yake ya kutoka ligi ya chini ya kushinda VPL katika msimu wao wa kwanza.
Sijui, Mwambusi amekosa bahati gani, alishindwa mara mbili akiwa Prisons na wakati alionekana kutambulisha uwezo wake wa kutengeneza timu inayoshambulia vizuri na kufunga magoli nyumbani na ugenini, Azam FC ikatokeza mbele yake na kushinda ubingwa wao wa kwanza.
Msimu huu ilishuhudiwa kiwango cha chini kutoka kwa klabu kubwa za Yanga na Simba na ilikuwa wazi kutokana na soka lake City ilipaswa kuishinda Azam FC katika mbio za ubingwa lakini wakajikuta wakianza kuangusha pointi muhimu katika michezo wa mwisho tena katika uwanja wa nyumbani Sokoine.
Maneno mengi yalisemwa kuhusu ubingwa wa Azam FC huku mbinu za kusaka matokeo nje ya uwanja zikitajwa mara kwa mara. Lakini Mwambusi pia alitajwa kama sababu ya kuanguka kwa kikosi hicho mwishoni mwa msimu.

No comments